Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.DEC 14.2016 SAA 11:13 JIONI
Kocha Mkuu wa Azam Fc Zeben Hernandez akiwa na Wachezaji waliosaini kutoka kulia mwenye rasta ndiye Yakubu Mohammed, Joseph Mahundi na kushoto kabisa ni Stephan Kingue Mpondo. |
UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC,
unayofuraha kuutarifu umma kuwa leo mchana imefanikiwa
kuingia mkataba
na wachezaji watatu, beki wa kati Yakubu Mohammed, kiungo mkabaji
Stephan Kingue Mpondo na winga Joseph Mahundi.
Zoezi hilo la kuingiana mikataba limehudhuriwa na baadhi ya viongozi
wakuu wa timu wakiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu,
Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Meneja wa timu, Phillip
Alando.
Wakati Mohammed, 20, amesaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Aduana
Stars ya Ghana, utakaomuweka kwenye viunga vya Azam Complex hadi
Desemba 14, 2019 akiziba nafasi ya Pascal Wawa, huku Mpondo anayetokea
Coton Sports ya Cameroon, kwa upande wake akisaini mwaka mmoja.
Nyota hao wawili wamepewa rasmi mikataba baada ya kulivutia benchi la
ufundi la Azam FC kwenye majaribio waliyokuwa wakifanya ndani ya kikosi
hicho.
Katika kuongeza makali kwenye eneo la ushambuliaji, Azam FC
imemrejesha winga wake wa zamani aliyekulia Azam Academy, Mahundi,
ambaye amesaini miaka miwili akitokea Mbeya City, alipomaliza mkataba
baada ya kumalizika kwa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara (VPL).
Azam FC tunaamini ya kuwa ujio wa nyota hao, utazidi kuipa nguvu timu
yetu kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
(VPL) unaotarajia kuanza wikiendi hii, Kombe la Shirikisho (Azam Sports
Federation Cup) na Kombe la Shirikisho Afrika (CC) mwakani.
Hivyo mashabiki wa Azam FC wasiwe na wasiwasi waendelee kuisapoti
timu, kwani bado uongozi wa timu kwa kushirikiana na benchi la ufundi,
una nia ya dhati ya kuipeleka mbele timu kufikia kwenye mafanikio
yanayokusudiwa kwa kukiboresha kikosi kadiri inavyowezekana.
Wakati huo huo, Azam FC inapenda kuweka wazi taarifa ya kufikia
makubaliano ya kuachana na kiungo mkabaji raia wa Rwanda, Jean Baptiste
Mugiraneza ‘Migi’, ambaye amepata timu nchini Vietnam na muda wowote
kuanzia sasa atakwenda huko.
Azam FC inamtakia mafanikio mema Migi huko aendako na inapenda
kumkaribisha muda wowote atakapojisikia kurejea tena hapa na katika
kuziba nafasi yake tumeamua kumsajili Mpondo, ambaye alikuwa nahodha wa
timu ya Taifa ya Cameroon kwenye kikosi kilichoshiriki Fainali za
Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika nchini
Rwanda mwanzoni mwa mwaka huu.
ANGALIA PICHA
ANGALIA PICHA
Joseph Mahundi akikabidhiwa jezi |
0 Comments