Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.DEC 15.2016 SAA 12:53 JIONI
Duru la Pili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuanza
kesho Jumamosi Desemba 17 kwa michezo minne kabla ya
michezo mingine
minne kufanyika siku ya Jumapili Desemba 18, mwaka huu.
Katika mechi za kesho, Mabingwa watetezi wa taji hilo, Young Africans
SC ya Dar es Salaam itakuwa mgeni wa JKT Ruvu ya Pwani kwenye mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Licha ya kwamba mwenyeji wa mchezo huo ni JKT Ruvu ambayo uwanja wake
wa nyumbani mara nyingi huwa ni Mabatini ulioko Mlandizi, lakini kwa
mujibu wa Kanuni ya 6 (5) na (6) ya Ligi Kuu Bara, mechi zake za
nyumbani dhidi ya Simba, Young Africans na Azam FC, hufanyika Uwanja wa
Uhuru.
Michezo mingine ya kesho ni Kagera Sugar kuwa mgeni wa Mbeya City
kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Ruvu Shooting ya Pwani
itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini,
Pwani ilihali Mwadui ya Shinyanga itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza
kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.
Jumapili, Desemba 18, mwaka huu Mbao FC ya Mwanza itacheza na Stand
United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Ndanda
itakuwa mwenyeji wa Vinara wa Msimamo katika Ligi Kuu ya Vodacom, Simba
kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
African Lyon ya Dar es Salaam itaikaribisha Azam FC pia ya Dar es
Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru jijijini siku hiyo ya Jumapili wakati
Majimaji ya Songea itakuwa Mbeya kucheza na Tanzania Prisons kwenye
Uwanja wa Sokoine.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limetoa masharti kadhaa likitaka klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kufuata.
Masharti hayo, ni kwa klabu kutumia makocha wenye sifa kwa mujibu wa
kanuni ya 72 ya Ligi Kuu ya Vodacom. Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu ya
Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) na kwa mujibu wa kanuni hiyo,
makocha wanaopaswa kukaa kwenye benchi la Ligi kuu kwa msimu huu
wasipungue sifa ya kuwa na leseni B ya CAF.
Pia kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza na Pili, masharti ni lazima
makocha wawe na sifa za kuzinoa timu hizo ambazo zimeanishwa kwenye
kanuni za ligi husika.
Kadhalika, tunaagiza klabu kutotumia wachezaji wa kigeni au makocha
kama hawana vibali vya ukaazi na kufanya kazi kutoka Idara ya Uhamiaji
nchini iliyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
0 Comments