Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.JULY 1,2016 SAA 09:28 USIKU
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa
chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Bakari Nyundo Shime, amesema
hatarajii kuwa
na mabadiliko makubwa ya kikosi katika mchezo dhidi ya vijana Shelisheli
utakaopigwa kesho Jumamosi Julai 2, 2016 kwenye Uwanja wa Stade Linite mjini
Victoria.
“Timu haitakuwa na mabadiliko makubwa. Almost kikosi
kitakuwa ni kilekile cha Dar es Salaam kwa sababu nitampumzisha Job (Dickson
Nickson) tu katika mchezo wa kesho, na nafasi yake atacheza Enrick (Vitalis
Nkosi),” amesema Shime leo Julai 1, 2016 kabla ya kwenda kwenye mazoezi ya
mwisho yatakayofanyika Uwanja wa Linite.
Shime maarufu kwa jina la Mchawi Mweusi, amesema
anauchukulia mchezo huo kwa uzito uleule na kuongeza ana sababu za kiufundi na
kimbinu kumpumzisha Job katika mchezo wa marudiano kuwania nafasi ya kufuzu
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana, zitakazofanyika mwakani huko
Madagascar.
Kwa hali halisi ilivyo timu iko vema na ikathibitishwa
na Shime mwenyewe akisema: “Kikosi kiko vema kwa maana ya wachezaji wako vizuri
na kambi iko vizuri kwa sababu hakuna majeruhi.” Pia Daktari wa timu hiyo,
Shecky Francis Mngazija alithibitisha.
“Sioni kama kuna dalili zozote za hujuma na kimbinu
tumejipanga vema. Tumefuta matokeo ya Dar na tuko huku tunataka matokeo mapya.
Mbinu zangu siku zote ni ushindi wa nyumbani na ugenini,” amesisitiza.
Serengeti Boys ilitua kwenye Kisiwa cha Mahe uliko
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Visiwa vya Shelisheli jana Juni 30, 2016 majira
ya saa 11 jioni.
Timu hiyo iliyosafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la
Ethiopia ilisafiri salama na wachezaji wote 20 wakiwa na viongozi wanane,
walikuwa kwenye hali nzuri na kupokewa vema na wenyeji waliowaandalia usafiri
kutoka uwanjani hapo hadi Victoria- Mji Mkuu wa nchi hii na kufikia Hoteli ya
Berjaya Beau Vallon Resort iliko Kilometa 25 kutoka uwanja wa ndege.
Leo Julai mosi, itakuwa na mazoezi ya kipindi kimoja
tu kwenye uwanja huo kuanzia saa 10.30 jioni (saa 9.30 kwa saa za Tanzania au
Afrika Mashariki). Uwanja wa Stad Linite upo kilometa 10 kutoka hotelini.
Shime ana matumaini makubwa kuiondoa Shelisheli katika
mbio hizo baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza
uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumapili ya Juni 26, 2016.
Na ili iweze kufuzu, Serengeti Boys inahitaji kusimama
imara katika matokeo hayo ama kwa kupata sare ya aina yoyote, kushinda au
ikitokea kupoteza, basi isifungwe zaidi ya mabao 2-0.
Katika mchezo wa Dar es Salaam waliozifumania nyavu
walikuwa Nickson Kibabage, Ibrahim Abdallah na Ally Hussein ambaye alifunga kwa
penalti na kila mmoja amepania kufunga kama kocha akiwapa nafasi ya kuanza
katika kikosi cha kwanza.
Nyota waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm
Kabwili na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari,
Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally
Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.
Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi
Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Yassin
Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Rashid
Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima
Makame Vitalis.
Serengeti Boys ambayo inahudumiwa na TFF kwa asilimia
100 ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mechi hizo za kufuzu
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Shelisheli na Afrika Kusini
ambayo itapambana nayo baadaye mwezi ujao.
Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys
ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa
yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya
kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika
Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.
0 Comments