Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.OCT.21,2016 SAA 12:28 JIONI
Ligi ya Taifa na Wanawake itaanza Novemba 1, 2016 kama ilivyopangwa
awali kwa kushirikisha timu 12 zilizopangwa kwenye
makundi mawili yenye
majina ya ‘A’ na ‘B’. Kila kundi lina timu sita.
Timu za kundi A lina timu za Viva Queens ya Mtwara, Fair Play ya
Tanga, Mlandizi Queens ya Pwani pamoja na Mburahati Queens, Evergreen
Queens na JKT Queens za Dar es Salaam wakati kundi B zimo Marsh Academy
ya Mwanza, Baobab Queens ya Dodoma, Majengo Women ya Singida, Sisters FC
ya Kigoma, Kagera Queens ya Kagera na Panama FC ya Iringa.
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utachukua takribani wiki tatu kwa
makundi yote yaani hadi Novemba 20, mwaka huu na mzunguko wa pili
utaanza Januari 4, 2017 hadi Februari mosi, mwakani.
Michezo ya kwanza kwa kundi A itakuwa ni kati ya Viva Queens na
Mburahati Queens utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara;
wakati Fair Play itacheza na Evergreen ya Dar es Salaam kwenye Uwanja
wa Mkwakwani jijini Tanga ilhali JKT Queens ya Dar es Salaam itakuwa
wenyeji wa Mlandizi ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar
es Salaam.
Kwa upande wa Kundi B michezo ya kwanza itakuwa ni kati ya Marsh
Academy ya Mwanza itayoonyeshana kazi na Majengo Women FC ya Singida
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Sister ya Kigoma
itakuwa mwenyeji wa Panama ya Iringa kwenye Uwanja wa Tanganyika mjini
Kigoma ilihali Kagera Queens itakuwa mgeni wa Baobab ya Dodoma kwenye
Uwanja wa Jamhuri mjini humo.
Ligi hiyo inakwenda kuanza ikiwa na mdhamini mmoja tu ambaye Kituo
cha Azam Tv ambacho kitaonyesha michezo yote bure kupitia king’amuzi
chake cha Azam.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatangaza kuwa kungali
na fursa ya kudhamini ligi hiyo kutoka kwa watu binafsi na kampuni
mbalimbali ambazo zitapata kutangazika wakati mechi za ligi hiyo
zikiendelea.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuandaa ligi hiyo kwa upande wa
wanawake ambako si tu kwamba itakuza kiwango cha soka kwa wanawake
nchini bali inatarajiwa kuleta hamasa mpya katika mapenzi ya mpira wa
miguu.
Pia benchi la ufundi la timu ya taifa kuweza
kugundua vipaji vipya vitakavyojumuishwa kwneye timu ya taifa ambayo
mwakani itaingia kwenye programu ya kuwania kucheza fainali za Kombe la
Dunia kwa wanawake kutoka kanda ya Afrika. Fainali za Kombe la Dunia kwa
wanawake zitafanyika mwaka 2019 huko Ufaransa.

0 Comments