Young Africans imeendeleza wimbi lake la ushindi kwenye michezo ya kirafiki baada ya leo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
timu ya Thika United katika mchezo uliofanyika jioni ya leo katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Ikicheza mchezo wa kwanza wa kimataifa mbele ya mashabiki wake jijini Dar es salaaam, kocha Maximo aliwaanzisha washambuliaji kutoka nchini Brazil Coutinho na Jaja wakisaidiwa na viungo kutoka nchini Rwanda Twite na Niyonzima na kiungo mzawa Dilunga.
Upande wa ulinzi mlinda mlango Deo Munish "Dida" alifanya kazi yake vizuri kwa kushirikiana na walinzi wa kati nahodha Nadir Haroub "Cannavaro" Kelvin Yondani na walinzi wa pembeni Juma Abdul na Oscar Joshua.
Thika Uinted ilicheza kwa kasi tangu mwanzo wa mchezo kwa lengo la kusaka la bao la mapema, lakini ukuta wa Young Africans ulikua imara na kuondoa hatari zote langoni.
Washambuliaji wa Young Africans hawakutengeneza nafasi nyingi za kufunga kipindi cha kwanza kutokana na winga wake Saimon Msuva kutokua makini katika kutoa pasi za mwisho, huku Coutinho akiwa mwiba mkali kwa walinzi wa Thika United.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwnaza zinamalizika, Young Africans 0 - 0 Thika United FC. Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko kwa lengo la kusaka mabao ya mapema, hali iliyopelekea mchezo kuchangamka na kuwa na ufundi mwingi.
Dakika ya 60 ya mchezo Geilson Santos "Jaja" alifanya kazi iliyomleta nchini baada ya kuukwamisha mpira wavuni, akitumia vizuri krosi ya winga Saimon Msuva aliyewatoka walinzi wa Thika United na kumpasia mfungaji ambaye hakufanya ajizi.
Baada ya bao hilo timu zote zilicharuka na kucheza soka safi, Thika United wakisaka bao la kusawazisha na Young Africans wakisaka kuongeza bao la pili, lakini mabadiliko yaliyofanyika kwa timu zote mbili hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 1- 0 Thika United.
Mara baada ya mchezo wa leo, kocha mkuu Marcio Maximo amesema vijana wake wamepambana kadri ya uwezo wao kuhakikisha wanapata ushindi, timu haikucheza vizuri sana lakini pia wageni Thika United wenzetu wapo kwenye Ligi inayondelea kuchezwa, tumepata kipimo kizuri kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu.
Young Africans: 1.Deo Munish "Dida", 2. Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4.Nadir Haroub "Cannavaro", 5.Kelvin Yondani, 6.Mbuyu Twite, 7.Hassan Dilunga/Hamis Thabit, 8.Haruna Niyonzima/Omega Seme, 9.Geilson Santos "Jaja"/Said Bahanuzi, 10. Saimon Msuva/Hussein Javu, 11. Andrey Coutinho/Nizar Kahlfani.
0 Comments