Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.JAN 14.2016 SAA 03:12 ASUBUHI
Azam Fc usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kutwaa taji la michuano ya Kombe
la Mapinduzi, ikiichapa Simba bao 1-0 katika
mchezo uliofanyika Uwanja
wa Amaan, Zanzibar.
Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, imetwaa taji hilo kwa
kuandika rekodi mpya na ya aina yake baada ya kutofungwa mchezo wowote
katika mechi tano ilizocheza za michuano hiyo, huku pia ikiwa
haijaruhusu bao lolote.
Azam FC ikicheza kwa ari kubwa na morali ya hali ya juu kwenye mchezo
huo, iliwachukua dakika 13 tu kuweza kuandika bao hilo la ushindi
lililofungwa kiufundi kwa shuti kali la umbali wa mita 25 na Nahodha
Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’.
Mao alipiga shuti hilo lililomshinda kipa wa Simba, Daniel Agyei,
kufuatia pasi safi aliyopigiwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Licha ya Simba kufanya mashambulizi kadhaa, ilijikuta ikutana na
upinzani mkali wa kuweza kuipenya safu ngumu ya ulinzi ya Azam FC chini
ya mabeki wa kati visiki, Aggrey Morris na Yakubu Mohammed.
Haikushangaza kusikia mwishoni mwa mchezo huo, Morris akitangazwa
kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kupewa zawadi ya katoni nne ya
kinywaji safi cha Azam Malti, kiatu cha kuchezea mpira na kikombe
maalum.
Azam FC kutwaa ubingwa huo, kumeifanya kujibebea kombe
walilokabidhiwa na mgeni wa heshima wa mchezo huo Rais wa Zanzibar, Dk.
Ali Mohammed Shein, pia walijizolea medali na kitita cha Sh. Milioni 10
na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, huku Simba wakipewa medali
za mshindi wa pili na Sh. Milioni 5.
Kamati ya mashindano hayo pia ilimtangaza kipa wa Azam FC, Aishi
Manula, kuwa Kipa Bora wa michuano hiyo, Beki Bora amekuwa ni Mzimbabwe
Method Mwanjali wa Simba na Mfungaji Bora ni Simon Msuva wa Yanga.
Taji la tatu
Ubingwa huo umeifanya Azam FC kuifikia rekodi ya Simba ya kulitwaa
taji hilo mara tatu, lakini mabingwa hao safari hii wakibebwa na rekodi
ya kulitwaa bila kufungwa mchezo wowote wala kuruhusu wavu wake kuguswa.
Mara mbili za nyuma, iliweza kuweka rekodi ya kuwa timu pekee
kulitwaa taji hilo mara mbili mfululizo, ikilibeba mwaka 2012 na 2013.
Rekodi zakolea Azam FC
Ubingwa huo unaifanya Azam FC kufikisha taji la pili msimu huu na hii
ni baada ya Agosti mwaka jana kutangulia kwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa
kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2
ndani ya dakika 90.
Hiyo ni rekodi ya pili mfululizo kwa Azam FC kutwaa taji bila
kuruhusu wavu wake kuguswa, itakumbukwa walifanya tena hivyo mwaka juzi
walipotwaa taji la kwanza la michuano ya Kombe la Kagame (CECAFA Kagame
Cup), ambapo kwenye fainali waliichapa Gor Mahia mabao 2-0.
Msimu wa 2013/2014, Azam FC ilifanya maajabu mengine ya kutwaa taji
la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) bila kufungwa
mchezo wowote.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa:
Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu
Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Himid Mao/Enock Atta Agyei dk
82, John Bocco, Yahya Mohammed/Mudathir Yahya dk 69, Joseph
Mahundi/Frank Domayo dk 57
0 Comments