Mabingwa wapya wa Kombe la Chalenji la CECAFA, timu ya taifa ya
wanawake ya Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro
Queens,
inatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam kesho Septemba 22, 2016 saa
7.00 mchana kwa ndege ya FastJet ikitokea Mwanza.
Mara baada ya kutua, itakwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya
Coartyard iliyoko Sea View, Upanga jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kupata chakula cha mchana ambako watakuwako viongozi wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wale wa Serikali akiwamo Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye ambaye pia
ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
Timu hiyo leo Septemba 21, 2016 ilitua Kagera ambako imetumia siku ya leo kuwafariji wahanga wa tetemeko la ardhi.
Itakumbukwa kwamba kabla ya kwenda Jinja, Uganda ambako ilivuna
ubingwa huo katika fainali zilizofanyika jana kwa kuilaza Kenya katika
fainali zilizofanyika Uwanja wa Njeru, Kilimanjaro Queens iliweka kambi
mjini Bukoba ambako ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya
Burundi na kushinda mabao 3-0 Septemba 8, mwaka kwenye Uwanja wa
Kaitaba.
Kilimanjaro Queens inatarudi Kagera kusema: “Ahsante” kwa wenyeji
akiwamo Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mstafu Salum Kijuu
aliyewakabidhi bendera kabla ya safari, lakini pia kuwapa pole Wahanga
wa janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na
mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika
zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.
Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa
usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo
kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu
hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Edna Lema
wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake, Amina Karuma.
Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa
kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo
pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia
zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika
kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-1 katika
mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa
mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya,
Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la
Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza
jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la
wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Wakati huo huo, timu ya taifa ya Vijana wa Tanzania wenye umri wa
chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kesho inatarajiwa kuondoka jijini
Dar es Salaam, Tanzania kesho Septemba 22, 2016 kwenda Kigali, Rwanda
kwa ajili ya kambi ya siku 10 kabla ya kuivaa Congo-Brazzaville katika
mchezo wa pili kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Baada ya Serengeti Boys kushinda
mabao 3-2, jijini Dar es Salaam, timu hizo zinatarajiwa kurudiana Oktoba
2, 2016 huko Congo Brazzaville na timu itafayopata ushindi wa jumla
katika michezo miwili itafuzu kwa fainali hizo.

0 Comments