Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.SEPT.20,2016 SAA 01:39 USIKU
Haikuwa ubashiri, badala yake ilikuwa ni mipango thabiti ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha kwamba
inavuna
ushindi na kuwa mabingwa wa Kombe la Chalenji la CECAFA kwa wanawake
baada ya kuilaza Kenya mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika
Uwanja wa Nambole jijini Jinja nchini Uganda.
Mabao ya timu ya taifa Tanzania ya wanawake maarufu kama Kilimanjaro
Queens katika mchezo wa leo Septemba 20, 2016 yamefungwa na Mwanahamisi
Omari katika kipindi cha kwanza kabla ya Kenya kujitutumua na kupata bao
la kufutia machozi kipindi cha pili katika mchezo uliokuwa na ushindani
wa aina yake.
Matokeo hayo yatakuwa kupozwa kwa ndugu zao wa Zanzibar Queens ambao
walitolewa mapema katika mashindano hayo yaliyoanza Septemba 11, 2016
kabla ya kufikia tamati leo katika fainali hizo zilizovutia mashabiki wa
mpira wa miguu nchini Uganda ambako kila upande ulikuwa na watu
wanaowasapoti.
Timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini Uganda kesho Jumatano na kwenda
moja kwa moja Kagera ambako ilipiga kambi kabla ya kwenda Jinja.
Itarudi hapo kusema ahsante kwa wenyeji, lakini pia kuwapa pole ya janga
la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa
jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi
ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.
Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa
usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo
kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu
hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Hilda Masanche
wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake.
Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa
kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo
pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia
zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika
kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-0 katika
mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa
mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya,
Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la
Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza
jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la
wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

0 Comments