Na.Boniface Wambura,IMEWEKWA FEB. 10,2014 SAA 09:46 ALASIRI
Kamati
ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia mechi tatu
wachezaji watano
kati ya tisa wa timu ya Kanembwa JKT waliolalamikiwa na
Sekretarieti kwa kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyochezwa
Novemba 2 mwaka jana.
Wachezaji
hao ni Bariki Abdul, Mrisho Musa, Nkuba Clement, Nteze Raymond na Philo Ndonde.
Wachezaji ambao hawakutiwa hatiani kutokana na ushahidi dhidi yao
kutojitosheleza ni Abdallah Mgonja, Mbeke Mbeke, Ntilakigwa Hussein na Uhuru
Mwambungu.
Mechi
hiyo dhidi ya Stand United iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga
ilivunjwa na refa Peter Mujaya dakika ya 87 kutokana na kupigwa na wachezaji
hao baada ya kuamuru ipigwe penalti dhidi ya timu yao.
Adhabu
hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 49 (1)(b) ya Kanuni za Nidhamu za TFF
baada ya kupitia vielelezo vilivyowasilishwa na Sekretarieti ya TFF ambavyo ni
ripoti ya refa, ripoti ya kamishna wa mechi hiyo na video iliyoonesha tukio
hilo.
Pia
kabla ya kutoa adhabu baada ya kusikiliza utetezi kutoka kwa walalamikiwa ambao
ni wachezaji hao na timu yenyewe ya Kanembwa JKT. Nayo Kanembwa JKT imetiwa
hatiani na kupigwa faini ya sh. milioni ambayo inatakiwa kuilipa kabla ya
kucheza mechi inayofuata.
Kamati
hiyo iliyokutana jana (Februari 9 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Tarimba
Abbas, kwanza imelaani kitendo cha wachezaji wa timu hiyo kumzonga refa, kwani vitendo
vya aina hiyo ndiyo vichocheo vya vurugu viwanjani.
Lakini
pia imempongeza nahodha wa Kanembwa JKT, Mbeke Mbeke kwa kuwa mstari wa mbele
kuwazuia wachezaji wenzake waliokuwa wakimpiga refa wa mchezo huo.
Vilevile
Kamati hiyo imesema aliyesababisha matatizo hayo ni refa Mujaya, na ingawa
ilikuwa na uwezo wa kumchukulia hatua lakini haikufanya hivyo kwa vile hakukuwa
na mlalamikaji na tayari Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilishamwadhibu.
MAJINA YA
MABINGWA WA MIKOA MACHI 30
Vyama
vya Mpira wa Miguu vya mikoa vimetakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao
kufikia Machi 30 mwaka huu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Timu
zote zitakazofuzu kucheza RCL zinaruhusiwa kusajili wachezaji wapya wasiozidi
watano kutoka ndani ya mkoa kwa kufanya taratibu za uhamisho. Kamati
imesisitiza kuwa usajili wa RCL ni uleule uliotumika kwenye Ligi ya Mkoa.
Kamati
ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
Februari 6 mwaka huu imekataa ombi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza
(MZFA) kuongeza timu za Ligi ya Mkoa kutoka 20 hadi 24.
Ikiwa
chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange, Kamati hiyo imesema kwa mujibu wa
Kanuni ya Ligi ya Mkoa, ligi hiyo inatakiwa kuwa na timu kati ya 16 na 20,
hivyo vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vinatakiwa kuendesha ligi kwa kufuata
kanuni.
Kamati
hiyo imeongeza kuwa hata kama ingekubalia ombi la MZFA kiutaratibu lisingewezekana
kwa vile kanuni hufanyiwa marekebisho baada ya msimu kumalizika, wakati ombi
hilo limewasilishwa katikati ya msimu.

0 Comments