Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba Jaji Joseph Warioba amesema Tume yake haishawishi wananchi wakubali
mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba waliyoiandaa kama inavyodaiwa na
baadhi ya watu lakini hulazimika kutoa ufafanuzi pale inapohitajika.
| Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba,wa kwanza kushoto |
Jaji Warioba alitoa ufafanuzi huo
mjini Morogoro jana (Jumamosi, Agosti 17, 2013) wakati akijibu swali la mmoja wa
Wajumbe wa Baraza la Katiba la Manispaa ya Morogoro aliyeomba ufafanuzi wa Tume
kuhusu kauli za baadhi ya wanasiasa kuwa Tume yake inashawishi Wajumbe wa
Mabaraza kukubali rasimu ya Katiba.
“Mna haki ya kuuliza na kupata
ufafanuzi na sisi kama Tume tuna wajibu wa kutoa ufafanuzi kwa yale mnayouliza
katika mikutano … huo sio ushawishi ni ufafanuzi,” alisema Mwenyekiti huyo
akijibu swali la mjumbe huyo Bw. Dotto Rangimoto.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Wajumbe
wa Tume wanaoendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba nchini huulizwa maswali
mbalimbali na wananchi wanaohudhuria mikutano hiyo wakitaka ufafanuzi wa mambo
mbalimbali yaliyomo katika rasimu ya katiba.
“Tusipojibu tutakuwa watu wa ajabu
sana,” alifafanua Mwenyekiti huyo katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa
Chuo cha Ualimu Kigurunyembe mjini Morogoro.
Ufafanuzi
wa Itikadi ya Ujamaa ndani ya Katiba
Katika mkutano huo, Jaji Warioba pia
alifafanua kuhusu misingi ya ujamaa na kujitegemea katika rasimu ya katiba
iliyoandaliwa na Tume yake.
Jaji Warioba amesema Tume yake
imependekeza katika rasimu ya katiba uwepo wa Dira na Malengo ya Taifa ambayo yatapaswa
kutekelezwa na serikali ya chama chochote kitakachokuwa madarakani.
“Ujamaa ni itikadi lakini kujitegemea
sio itikadi … na baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa,
tulikubaliana kuwa vyama vitakuwa na itikadi tofauti,” alisema Mwenyekiti huyo
na kufafanua kuwa mapendekezo ya Tume yake yanalenga kutekeleza malengo ya
taifa na sio itikadi ya chama chochote kitakachokuwa madarakani.
Ufafanuzi wa Jaji Warioba ulitokana
na swali la Mjumbe wa Baraza hilo Bw. Andrew Tarimo aliyetaka kujua itikadi ya
inayopendekezwa na Tume baada ya ile ya ujamaa na kujitegemea kuondolewa katika
rasimu iliyoandaliwa na Tume na kuzinduliwa Juni 3 mwaka huu.
“Rasimu imeweka dira na malengo
ambayo yatasimamiwa na chama chochote bila kujali itikadi ya chama hicho,”
alisema.
Baraza la katiba la Manispaa ya
Morogoro limemaliza mkutano wake wa siku tatu jana (Jumamosi, Agosti 17, 2013) uliohudhuriwa
na wananchi 155 kutoka kata 29 za Manispaa hiyo. Keshokutwa (Jumatatu, Agosti
19, 2013), Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro nalo linatarajiwa kuanza
mkutano wake wa siku tatu kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya
katiba.
0 Comments