Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.OCT.5,2016 SAA 01:04 USIKU
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu,
Bunge na Vijana, Dk. Abdallah Possi amesema kwamba
Serikali itaendelea
kusapoti michezo kwa sababu ya umuhimu wake, lakini akataka kutafutwa
mbinu za kuhakikisha wadhamini wanasapoti timu za taifa na klabu
mbalimbali zinazoshiriki ligi zinazosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF).
Dk. Possi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwapongeza vijana wa
Timu ya Taifa ya Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti
Boys’, alisema kwamba fursa ipo ya kufanya vema katika michezo na ndiyo
maana Serikali inasapoti michezo kwa sababu ya kuleta faraja,
kuunganisha au kuleta umoja katika nchi yoyote kadhalika ni ajira.
Dk. Possi aliyesifu juhudi za TFF na timu hiyo, aliwapoza vijana hao
akiwaeleza kuwa “Juhudi zilifanyika na mnaona kiwango kilichotumika
kuandaa timu yenu. Matokeo mliyopata ndiyo mchezo. Kushindwa haina maana
tumeishia hapa,” alisema Dk. Possi alipokuwa akiwapongeza vijana hao
katika hafla hiyo iliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Ili kuepuka gharama kubwa za kuendesha timu hizo ambako Serengeti
Boys imetumika karibu bilioni moja, Dk. Possi amesema kwamba
kunahitajika kutengenezwa mfumo wa kupata wadhamini ili baadaye bidhaa
za TFF zigombaniwe na hata kampuni zinazofanya biashara inayofanana
zinaweza kuingia kudhamini katika ligi moja au klabu kwa sababu zitavuna
maslahi.
Akiwageukia wachezaji, Dk. Possi alisema wachezaji hawana budi kuwa
na nidhamu ya hali ya juu si katika kuonyesha kusabahi tu, bali kutunza
mwili. “Mtafika mbali kama mkiwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja. Mna
walimu, mna viongozi, ni vema mkawa mnawasikiliza wengine,” alisema Dk.
Possi huku akitaja majina ya nyota waliofanikiwa kwa kuwa na nidhamu na
wengine ambao walioanguka kwa kuwa na nidhamu mbovu.
Kabla ya kumkaribisha Dk. Possi, Rais wa TFF Jamal Malinzi alianza na
kutoa taarifa ya matokeo huko Congo Brazzaville, akisema: “Ilikuwa siku
mbaya sana kwangu. Watoto walikwenda kufia nchi. Lakini jahazi
halijafika mwisho, kuvunjika kwa mpini, sio mwisho wa uhunzi. Userengeti
Boys unakwisha na sasa unakuja Ungorongoro Heroes timu ya taifa ya
vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.”
Malinzi aliyetumia nafasi hiyo kumpa nafasi tena Kocha Mkuu wa vijana
hao, Bakari Nyundo Shime alisema kikosi hicho kinapambana kucheza
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2019 na ili kujindaa timu
hiyo inatarajiwa kwenda Korea Kusini kwenye mashindano maalumu
itawasaidia kuongeza uwezo wenu, kutembea na kutafuta soko la kimataifa
la soka.
Alisema kwamba mara baada ya timu hiyo kurejea, itakuwa inakusanhyika
kila baada ya miezi mitatu ili kufanya mazoezi ya pamoja na kupata
mchezo angalau mmoja wa kirafiki huku akitangaza kuwa vijana wa Mwanza,
wanaosoma katika shule ya Alliance wanatarajiwa kuunda kikosi kipya cha
timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
“Timu ile ya Mwanza ambayo kwa sasa ina vijana wa chini ya miaka 15,
ndio watakaounda kikosi cha fainali za vijana ambazo zitafanyika hapa
nchini mwaka 2018. Desemba watoto wale watacheza mechi ya kwanza ya
kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, ambako watapigiwa wimbo wa taifa,”
alisema Malinzi na kuongeza kuwa vijana walioibuliwa kutoka michuano ya
Airtel Rising Stars nao watajumuishwa.
“Ligi ya wanawake inayokuja. Ndiyo nayo itazaa timu bora ya wanawake
ambayoi itashiriki fainali za Kombe la Dunia hapo mwaka 2019. Ili tuweze
kufanya yote haya, tunahitaji fedha na tayari tumeanzisha mfuko maalumu
wa kuchangia timu hizi unaitwa TFF Fund ambao utakuwa na mtendaji wake
na ofisi yake,” alisema na kuongeza, “Yote haya yanalenga Tanzania
kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2016.”






0 Comments