Ticker

6/recent/ticker-posts

FAHAMU WACHEZAJI WATATU WALIOOMBEWA ITC KWENDA UJERUMANI,MAPATO YA MECHI YA JANA KATI YA AZAM FC NA MBEYA CITY NA MICHUANO YA UHAI CUP

 IMEWEKWA NOVEMBA 8.2013 SAA 09:31 MCHANA

Watanzania watatu wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB) ili wacheze mpira wa miguu nchini humo.
Wachezaji hao ni Charles Mishetto na David Sondo wanaombewa hati hiyo ili waweze kujiunga na timu ya SpVgg 1914 Selbitz, wakati Eric Magesa ameombewa kibali hicho ili achezee timu ya klabu ya SC Morslingen.

Hata hivyo, katika maombi hayo DFB haikuleza hapa nchini walikuwa wakicheza katika klabu zipi. Wachezaji wote wameombewa hati hiyo kama wachezaji wa ridhaa.

MECHI YA JKT RUVU, COASTAL YAINGIZA LAKI 2/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji JKT Ruvu na Coastal Union ya Tanga iliyochezwa juzi (Novemba 6 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam imeingiza sh. 201,000.

JKT Ruvu iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi hiyo namba 85 na kushuhudiwa na watazamaji 67 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 3,000 na 10,000.

Kila klabu ilipata mgawo wa sh. 39,010 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 30,661.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 19,835, tiketi sh. 38,100, gharama za mechi sh. 11,901, Bodi ya Ligi sh. 11,901, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,950 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,628.

Nayo mechi kati ya Ashanti United na Simba iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa imeingiza sh. 24,931,000 ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 5,333,590.

Wakati huo huo, mechi za jana (Novemba 7 mwaka huu) kati ya Yanga na Oljoro imeingiza sh. 34,902,000 kutokana na watazamaji 6,045 ambapo kila klabu imepata sh. 7,812,477.95. Mechi ya Azam na Mbeya City iliyochezwa Azam Complex yenyewe imeingiza sh. 15,973,000 kwa watazamaji 4,857 na kila klabu imepata sh. 3,953,162.

UHAI CUP KUANZA KUTIMUA VUMBI NOV 17
Michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu inaanza kutimua vumbi Novemba 17 mwaka huu katika viwanja vya Karume na Azam Complex, Dar es Salaam.

Droo ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Maji Uhai imefanyika leo (Novemba 8 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo timu zimepangwa katika makundi matatu.

Kundi A linaundwa na timu za Azam, Coastal Union, JKT Ruvu Stars, Mbeya City na Yanga, wakati kundi B ni Ashanti United, Mgambo Shooting, Oljoro JKT na Ruvu Shooting. Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Rhino Rangers na Tanzania Prisons ndizo zinazounda kundi C.

Mechi za ufunguzi kundi A Novemba 17 mwaka huu ni kati ya Azam na Coastal Union (saa 2 asubuhi- Karume), Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Karume). Kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United (saa 4 asubuhi- Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Karume).

Kagera Sugar na Mtibwa Sugar (saa 2 asubuhi- Azam) na Rhino Rangers na Tanzania Prisons (saa 10 jioni- Azam) ndizo zitakazocheza mechi za ufunguzi Novemba 17 mwaka huu katika kundi C.

Robo fainali ya michuano hiyo itachezwa Novemba 24 na 25 mwaka huu wakati nusu fainali itapigwa Novemba 26 na 27 mwaka huu. Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na ile ya fainali zitachezwa Novemba 30 mwaka.


Post a Comment

0 Comments