Imezibitishwa na Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage kuwa klabu ya simba imefanikiwa kumuunganisha mchezaji wake, Shomari Salum Kapombe, na klabu ya soka ya AS Cannes ya Ufaransa.
Katika mkataba huo mpya na wa aina yake kuwahi kufanywa na
klabu yoyote ya Tanzania, Simba imekubali mchezaji huyo achezee timu hiyo iliyo
katika ligi daraja la nne la Ufaransa kwa
makubaliano ya kumtafutia timu ya kucheza ndani ya miaka miwili kutoka sasa.
makubaliano ya kumtafutia timu ya kucheza ndani ya miaka miwili kutoka sasa.
Timu hiyo itamgharimia Kapombe kwa kila kitu wakati
atakapokuwa nchini Ufaransa. Endapo Kapombe atauzwa kwenda katika timu nyingine
yoyote, Simba itapata gawio lake kupitia mauzo hayo na lengo la mchezaji huyo
kubaki Ufaransa ni pia kumtengeneza awe bora zaidi kuliko alivyo sasa.
“Kwenye makubaliano hayo, Simba haitapata chochote kwa sasa.
Isipokuwa endapo Kapombe atapata timu, Simba itapata mgawo wake kutoka katika
mauzo hayo. Makocha wa Ulaya wamebaini kwamba Shomari ni mchezaji mzuri sana
lakini anahitaji kuboreshewa vitu vichache kabla hajawa mchezaji mkubwa wa
kutumainiwa na vilabu vikubwa,” alisema Rage.
Rage alisema katika mkataba huo mpya wa Kapombe, Simba
imeangalia zaidi maslahi ya taifa na ya mchezaji kuliko ya klabu kwa vile kama
mchezaji huyo atapata nafasi Ulaya, hilo litafungua milango kwa wachezaji wengi
wa Kitanzania ambao kwa sasa hawapati fursa Ulaya.
Wakala wa Kapombe, Denis Kadito, alisema ingawa Kapombe
ameonekana kuwa mchezaji mzuri, kutofahamika kwa jina la Tanzania kumekuwa
kikwazo kikubwa kwa kupata kwake nafasi ya moja kwa moja na ndiyo maana imebidi
aanzie kwenye hatua ya chini.
“Ofa hii ya Cannes ni nzuri kwa sababu timu hiyo huwa
inacheza na timu za akiba za vilabu vyote vinavyoshiriki katika Ligi Kuu ya
Ufaransa na hivyo atakuwa anaonwa na mawakala wa timu kubwa kila wiki. Hii
itamsaidia kupata timu kubwa mapema ndani ya msimu mmoja kutoka sasa,” alisema
Kadito.
AS Cannes ni mojawapo ya vilabu vikubwa nchini Ufaransa na
ni maarufu kwa kuibua vipaji vikubwa. Miongoni mwa nyota maarufu wa Ufaransa
waliowahi kupita katika klabu hiyo ni Patrick Vieira, Zinedine Zidane na Luis
Hernandez.
Klabu hiyo inafahamika kwa kuwa na miundombinu imara ya
kumwezesha mwanasoka kijana kukuza uwezo wake na ni matarajio ya Simba Sports
Club, Kadito, Cannes na Kapombe mwenyewe kwamba atakuwa mchezaji bora zaidi
kuliko sasa katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka sasa.
Kutokana na mkataba huo wa Kapombe na Cannes, Simba sasa
imeongeza mkataba wake na mchezaji huyo kwa muda wa miaka mitatu zaidi, kwa
vile mkataba wake wa sasa unamalizika Aprili mwakani. Kama Kapombe hatafanikiwa
kupata timu katika kipindi cha miaka miwili kutoka sasa, atarejea katika klabu
ya Simba kuendelea na majukumu yake.

0 Comments