UONGOZI
wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, umetangaza rasmi
kuwatema wachezaji sita kwa awamu ya
kwanza huku nyota wawili wakifeli
majaribio.
Nyota hao walioachwa ni makipa Ivo Mapunda, Khalid Mahadhi aliyekuwa
ametolewa kwa mkopo Mafunzo ya Zanzibar, mabeki Said Morad, Racine Diouf
kutoka Senegal pamoja na washambuliaji Didier Kavumbagu (Burundi) na
Allan Wanga (Kenya).
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, alisema wachezaji hao wameachwa
wakiwa wamepata stahiki zao kwa wale ambao waliokuwa wamebakiwa na
mikataba.
Alisema mbali na wachezaji hao, pia wachezaji wawili kati ya wanne
waliokuwa kwenye majaribio nao wameachwa rasmi ambao ni beki wa kushoto
kutoka Ghana, Nurudeen Yusif aliyetokea Medeama ya huko na kiungo
mshambuliaji David Wirikom (Cameroon).
Wawili hao wamepewa majibu ya kufeli majaribio yao leo asubuhi
kufuatia Kocha Mkuu Zeben Hernandez, kutoridhishwa na uwezo wao kwa siku
nne walizofanya mazoezi na kikosi cha Azam FC.
“Wakati tunajiandaa na msimu mpya kuna wachezaji tuliwaalika kutoka
nchi mbalimbali Afrika kwa ajili ya kufanya majaribio, ambao mpaka sasa
wapo wanne, tangu tulipoanza mazoezi kwa siku takribani nne mwalimu leo
ameamua kuwapunguza wawili na wawili wamebakia.
“Waliofeli majaribio ni David Wirikom kutoka Cameroon na Nurudeen
Yusif kutoka Ghana, kocha ameona viwango vyao havitofautiani sana na
viwango vya wachezaji wetu hapa nyumbani, kocha ameongea nao leo mara
baada ya mazoezi na kuwaambia haoni kama wanaweza kumsaidia kwa sababu
anataka kuona mtu wa kimataifa anayekuja awe zaidi ya wachezaji wetu,”
alisema.
Wachezaji wanaoendelea kwenye majaribio ni makipa Daniel Yeboah
(Ivory Coast) na Juan Jesus Gonzalez (Hispania), ambao wanawania nafasi
moja ya usajili katika eneo la golikipa.
Jaffar alimalizia kwa kusema kuwa wanatarajia kuwapokea wachezaji
wengine wa kimataifa ndani ya siku mbili au tatu zijazo kwa ajili ya
majaribio yote ni katika kuendelea.
0 Comments