(Kushoto ) KIPA kutoka nchini Hispania, Juan Jesus Gonzalez akiwa na Ofisa Habari wa Azama Fc Jaffar Idd |
KIPA kutoka nchini Hispania, Juan Jesus Gonzalez, ametua nchini leo
mchana tayari kabisa kufanya majaribio ya kujiunga na Klabu
Bingwa ya
Afrika Mashariki na Kati Azam FC.
Siku chache zilizopita MAKOCHA
wapya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC kutoka nchini
Hispania, walitua rasmi jijini Dar es Salaam tayari
kabisa kuanza maandalizi ya msimu ujao (2016-17).
Wakufunzi hao waliotua na kupokelewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Azam FC, Saad Kawemba, pamoja na Ofisa Habari Jaffar Idd, ni Kocha Mkuu
Zeben Hernandez na Msaidizi wake Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo
Jonas Garcia na Msaidizi wake, Pablo Borges na Kocha wa Makipa Jose
Garcia.
Jopo hilo la makocha litaongezewa nguvu na makocha wengine wazawa
waliokuwa na Azam FC msimu uliopita, Kocha Msaidizi Dennis Kitambi na wa
Makipa, Idd Abubakar.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
mara baada ya kutua kwa mara ya pili nchini Kocha Mkuu Zeben, alisema
wamekuja kuanza rasmi kazi kuanzia Jumatatu Ijayo (Julai 4, 2016) kwenye
Makao Makuu ya Azam Complex, Chamazi.
Kocha huyo wa zamani wa CD Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa
kabla ya kuanza kazi rasmi Jumatatu, kesho Jumapili wanatarajia kukutana
na uongozi wa Azam FC pamoja na kutembelea makao makuu ya Azam
Complex.
Daktari kutua Julai 12
Katika hatua nyingine alisema kuwa Daktari wa timu hiyo, Sergio
Perez, anatarajia kutua nchini Julai 12 mwaka huu, na hawakuweza kutua
naye leo kutokana na kumalizia baadhi ya mambo na timu yake anayofanya
kazi kwa sasa.
Tayari Zeben ameshaweka wazi kuwa jambo kubwa analokuja kulifanya
Azam FC ni kuifanya timu hiyo ipate matokeo mazuri na kutisha barani
Afrika ikiwa inacheza soka safi la kisasa lenye muoanekano wa
Kihispania.
C.E.O afafanua ujio wao
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa
makocha hao wanatarajia kuanza programu yao wiki ijayo huku kesho
(Jumapili) wakitarajia kufanya nao kikao kwa ajili ya kujipanga na msimu
ujao.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu baada ya makocha wetu kufika salama,
kama tulivyopanga kesho watakuwa na kikao na uongozi, baada ya hapo
wataanza rasmi programu yao Jumatatu na hapo ndipo tutakuwa tunaanza
maandalizi ya msimu ujao,” alisema.
Kucheza mechi za Kimataifa
Kawemba alisema kuwa katika maandalizi yao wamejipanga kuwatafutia
makocha hao mechi za kirafiki za Kimataifa, endapo hakutakuwa na
michuano ya Kombe la Kagame walilolitwaa mwaka jana kwa kuwachapa
mabingwa wa Kenya Gor Mahia mabao 2-0.
“Baada ya mazoezi hayo tunatarajia uwepo wa michuano ya Kombe la
Kagame tukiwa mabingwa watetezi, kama haitakuwepo tumejipanga kutafuta
mechi za kirafiki za Kimataifa kwa ajili ya kuiweka vizuri timu yetu kwa
ajili ya msimu ujao na tunaamini ya kuwa utakuwa ni msimu wa mafanikio
kwa upande wetu,” alisema.
Nyota wa kimataifa kutua
“Tunatarajia wiki ya kwanza ya mazoezi yetu watakaohudhuria watakuwa
ni wachezaji wetu tuliokuwa nao msimu uliopita, ila tunatarajia
kuwapokea wachezaji kadhaa wa kimataifa watakaokuja kwa majaribio hao
wataanza kuingia nchini kuanzia Alhamisi ijayo na makocha wetu
watatuambia ni wachezaji gani wanaowahitaji kuwasajili kwa msimu ujao,”
alisema bosi huyo wa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB.
Awatoa hofu mashabiki
Kutokana na Azam FC kuwa kimya kwenye zoezi la usajili linaloendelea
hivi sasa, Ofisa huyo aliwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kuwaambia
kuwa mambo mazuri yanakuja kuelekea msimu ujao.
“Tunawaomba mashabiki wa Azam FC wawe watulivu katika kipindi hiki,
na nawaomba kwa wale wa karibu na Azam Complex wajitokeze kwa wingi
kuanzia Jumatatu kushuhudia maandalizi yetu,” alisema.
Makocha hao wanatua nchini kuziba nafasi za benchi la ufundi
lililopita la Azam FC chini ya Stewart Hall, Msaidizi wake Mario
Marinica na Mtaalamu wa Viungo, Adrian Dobre, waliojiuzulu kuinoa timu
hiyo mara baada ya mchezo dhidi ya JKT Ruvu (2-2) msimu uliopita.
0 Comments