Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), leo Juni 7, 2016 limefanya kikao cha pamoja na uongozi wa Klabu ya
Young Africans.
Kikao hicho kilifanyika ofisi ya TFF iliyoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Rais wa TFF Jamal Malinzi kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine; Kaimu Mkurugenzi wa Sheria na Uanachama, Elliud Mvella; Makamu Mwenyekiti wa Young Africans, Clement Sanga na Katibu Mkuu wa Young Africans, Baraka Deusdedit.
Baada ya mazungumzo, Rais wa TFF, Malinzi ametoa maelekezo yafuatayo:-
1. Mchakato wa Uchaguzi wa Young Africans uendelee.
2. Mchakato huo usimamiwe na Kamati ya Uchaguzi ya Young Africans chini ya uangalizi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
3. Wale wote waliochukuliwa fomu za uchaguzi wa Young Africans katika ofisi za TFF washirikishwe kwenye mchakato huo.
Mwisho, Rais wa TFF Jamal Malinzi amewatakia kila la kheri wanachama na wapenzi wa Young Africans na kuwa na umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi huo muhimu wa kwa mustakabali wa klabu.
TFF YATEUA KAMATI YA LESENI ZA KLABU
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeteua Kamati ya Leseni (Club Licensing Committee) ambayo ndiyo yenye jukumu la kupitia maombi ya leseni kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza na kutoa uamuzi kwa kuzingatia Kanuni ya Leseni ya Klabu.
Wajumbe walioteuliwa kwenye Kamati hiyo inayoundwa kwa mara ya kwanza ni Wakili Lloyd Nchunga (Mwenyekiti), Wakili Emmanuel Matondo (Makamu Mwenyekiti), David Kivembele, Hamisi Kissiwa na Prof. Mshindo Msolla.
Klabu zinatakiwa kuchukua fomu za maombi TFF ambapo baada ya kuzirejesha zitafanyiwa kazi ambapo zile zitakazokuwa zimekidhi matakwa ya Kanuni husika zitapatiwa leseni husika ili zishiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kwa msimu wa 2016/2017.
Kwa klabu ambazo zitashindwa kukidhi matakwa ya leseni yanayolenga kuhakikisha mpira wa miguu unaendeshwa kwa weledi na kupiga vita upangaji matokeo katika maeneo matano ya wachezaji (sporting), viwanja (infrastructure), utawala (administrative and personnel), umiliki wa klabu (ownership) na fedha (financial), hazitapa leseni hivyo kutokuwa na sifa ya kushiriki ligi.
Klabu ambazo zitanyimwa leseni na kutoridhika na uamuzi huo, zitakuwa na fursa ya kukata rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF. Kwa mujibu wa Ibara ya 5(3) ya Kanuni ya Leseni ya Klabu ya TFF, Kamati hiyo ndiyo inayosikiliza rufani zinazopinga uamuzi wa Kamati ya Leseni ya TFF.
Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ni Wakili Alloyce Komba (Mwenyekit), Wakili Abdallah Gonzi (Makamu Mwenyekiti), Dk Francis Michael, Abdallah Mkumbura na Wakili Twaha Mtengela. Klabu zote zinahimizwa kuchukua fomu za maombi mapema ili kutoa muda wa kutosha kwa TFF kupitia maombi yao na kufanya uamuzi kwa wakati muafaka.
KWA TAARIFA,BREAKING NEWS,RATIBA PAMOJA NA MATOKEO YA MECHI MBALIMBALI,LIKE PAGE YA FACEBOOK BONYEZA HAPA (Jamii na Michezo) .

0 Comments