Ticker

6/recent/ticker-posts

KAVUMBAGU KUJIUNGA NA MBEYA CITY

   Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.Jun 8,2016 SAA 12:49 JIONI

NYOTA wa timu ya Taifa ya Burundi ‘Intamba Mu rugamba’ Didier Kavumbagu anaweza kuwa mchezaji wa kwanza
kutangazwa kujiunga na kikosi cha Mbeya City Fc ya jijini Mbeya kinachoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara muda wowote kuanzia sasa.

Katibu Mkuu wa City, Emmanuel Kimbe, mchana huu ameidokeza mbeyacityfc.com kuwa mazungumzo ya kumnasa nyota huyo wa timu ya taifa ya Burundi aliyekuwa akicheza kwenye kikosi cha Azam Fc ya jijini Dar es Salaam msimu uliomalizika yako kwenye hatua nzuri na tayari wakala wa mchezaji huyo amekwisha ainisha yale yote muhimu yanayohitaji kwa ajili ya kuipata huduma yake likiwemo suala la kipengere cha kumruhusu kwenda kufanya majaribio nje ya nchi endapo yatapatikana.

“Tulianza mchakato wa kumpata Kavumbagu mapema kabisa, baada ya kukwama kwenye dirisha dogo mwezi januari, tulikubaliana kuwa hitimisho litakuwa kwenye majira haya ya kiangazi, tayari nimezungumza na wakala wake,tuko kwenye hatua za mwisho kwa sababu ameshaanishia yale yote yanayohitajika, kwa maana hiyo basi,endepo tutamalizia vizuri hatua iliyobaki,muda wowote kuanzia sasa tunaweza kumtangaza kama mchezaji wetu ” alisema.

Akiendelea zaidi Kimbe alisema kuwa Kavumbagu ni moja ya nyota walio kwenye orodha ya kocha Kinnah Phiri aliyoomba wasajiliwe ili kuiimarisha timu kwenye eneo la ushambuliaji akilenga kuwa wachezaji wenye uwezo wa kufunga kufuatia tatizo la umaliziaji lililoikuba City kwenye michezo kadhaa ya mzunguko wa pili wa ligi licha ya kucheza vizuri kwenye maeneo mengine.

“Tunayo majina kadhaa ambayo kocha wetu ameomba wasajiliwe kulingana na mahitaji aliyonayo, Kavumbagu anaweza kuwa wa kwanza kati yao,wengine watafuata kwa mujibu wa taratibu zetu, tunataka kufanya usajili makini ili kuimarisha timu na hatimaye tuwe na kikosi kitakachotupatia matokeo mazuri msimu ujao hii ni baada ya mapito msimu uliopita”.

Kavumbagu alianza kuichezea timu ya taifa ya Burudi mwaka 2009 na alikuwa mmoja wa nyota waliokiwakilisha kikosi hicho kwenye michezo ya kutafuta kufuzu kombe la Mataifa Afrika mwaka 2012 na kufunga mabao 2.

Kwa upande mwingine Kimbe amedokeza kuhusu nyota ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha City msimu ujao, na kusema kuwa ni vizuri kuendelea kusubiri kwa sababu muda si mrefu taarifa juu ya hilo itatolewa.

CHANZO:mbeyacityfc.com

KWA TAARIFA,BREAKING NEWS,RATIBA PAMOJA NA MATOKEO YA MECHI MBALIMBALI,LIKE PAGE YA FACEBOOK  BONYEZA HAPA (Jamii na Michezo) .

Post a Comment

0 Comments