IMEWEKWA FEB. 15,2014 SAA 01:01 USIKU
![]() |
Mrisho Ngasa akipokea zawadi ya mpira kutoka kwa mwamuzi wa mchezo wa leo kutoka Sychelles Allister Barra wa kufuatia kufunga mabao matatu (hat-trick) |
Wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Barani
Afrika timu ya Young Africans leo imeweza kufuzu raundi
ya pili ya
mashindano hayo kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya
wenyeji timu ya Komorozine de Domoni katika mchezo uliofanyika jioni ya
leo katika dimba la Uwanja wa Sheikh Said Ibrahim Mitsamihuli Comoro.
Ikicheza mbele ya Balozi wa Tanzania nchini Comoro Bw. Chabaka
Kilumanga Young Africans imefanikiwa kufuzu hatua ya pili ya Mashindano
ya Klabu Bingwa Barani Afrika kwa jumla ya mabao 12- 2, kufutaia ushindi
wa mabao 7-0 katika mchezo wa awali uliofanyika jijini Dar es salaam
huku Mrisho Ngasa akifunga "Hat-trick" katika michezo yote miwili.
Komorozine
de Domoni ikicheza mbele ya Gavana wa jimbo lao la Anjuani iliuanza
mchezo kwa kasi kwa lengo la kusaka bao la mapema ili kuwapa nguvu
washangiliaji wao amabo walikuja kuipa sapoti timu hiyo.
Hamis
Kiiza aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 13 ya mchezo
kufuatia kuitumia vizuri krosi ya mlinzi wa kushoto Oscar Joshua
aliyepanda kuongeza nguvu mashambulizi na pasi yake kumkuta Kiiza ambaye
aliukwamisha mpira wavuni bila ajizi.
Dakika ya 22 ya mchezo,
Mrisho Ngasa aliwainua mashabiki wa Young Africans vitini kufuatia
kuifungia timu yake bao la pili kufuatia migongeo mizuri ya Haruna
Niyonzima na Didier Kavumbagu.
Saimon Msuva aliipatia Young
Africans bao tatu kufuatia kufanya shambulizi langoni mwa timu ya
Komorozine de Domoni baada ya pasi za viungo Athuman idd, Haruna
Niyonzima na Mrisho Ngasa kumkuta mfungaji ambaye hakufanya makosa.
Dakika
ya 41 ya mchezo makosa ya mpira ulioptezwa na Hamis Kiziza
yaliwapelekea Komorozine de Domoni kijipatia bao la kwanza baada ya
mshmabuliaji wao kumtoka Oscar Joshua na kupiga krosi iliyomkuta
mfungaji.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika, Komorozine de Domoni 1 - 3 Young Africans.
Kipindi
cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Young Africans
iliwaingiza Frank Domayo, Hassan Dilunga na Said Bahanuzi waliochukua
nafasi za Athuman Idd, Saimon Msuva na Didier Kavumbagu mabadiliko
ambayo yaliongeza kasi ya mashambulizi.
Dakika ya 77 Korozine de
Domoni walijipatia bao la pili kufuatia makosa ya kiungo Hassan Dilunga
baada ya mpira alipoteza kunaswa na msahmbuliaji wa Komorozine na
kuwazidi ujanja walinzi wa Young Africans na kuukwamisha mpira wavuni.
Mrisho
Ngasa aliipatia Young Africans bao la nne dakika ya 87 ya mchezo
kufuatia Said Bahanuzi kuwatoka walinzi wa Komorozine na kupiga krosi
iliyomkuta Ngasa na kuukwamisha mpira wavuni kwa kifua.
Dakika ya
90 ya mchezo Mrisho Ngasa aliendelea kuwapa furaha tena washabiki wa
Young Africans waliojitokeza uwanjani leo kuishangilia timu yao baada ya
kuipatia timu yake bao la tano na la ushindi kwa kichwa baada ya
kuitendea vyema krosi ya kiungo Haruna Niyonzima.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Komorozine de Domoni 2 - 5 Young Africans.
Mara
baada ya mchezo mwamuzi wa mchezo wa leo Allister Barra alimkabidhi
mpira mshambuliaji Mrisho Ngasa kufuatia kufunga mabao 3 peke yake
(hat-trick) katika mchezo wa leo.
Baadhi ya watanzania
walijitokeza kuishangilia timu yao ya Young Africans wakiongozwa na
Balozi wa Tanzania nchini Comoro Chibaka Kilumanga walifurahishwa na
ushindi huo na kusema wamefarijika na timu yao kwa kushinda mchezo wa leo na kusema wanaitakia kila la kheri katika michezo inayofuata.
Kesho
mchana Msafara wa Young Africans umealikwa chakula cha mchana nyumbani
kwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro Bw.Ckibaka Kilumanaga na siku ya
jumatatu kikosi kitaanza safari ya kurejea nchini majira ya saa 6 mchana
kwa shirika la ndege Precision Air.
Young Africans:
1.Dida, 2.Twite, 3.Oscar, 4.Cannavaro, 5.Yondani, 6.Chuji/Dilunga,
7.Msuva/Domayo, 8.Niyonzima, 9.Didier/Bahanuzi, 10.Ngasa, Kiiza
CHANZO:www.youngafricans.co.tz
0 Comments