Ticker

6/recent/ticker-posts

TAARIFA MBILI KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA TANZANIA, ZISOME

 Na.Boniface Wambura,IMEWEKWA JANUARI 17,2014 SAA 12:12 JIONI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina ya siku mbili kwa makatibu wa vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa kuhusu maboresho ya timu ya Taifa (Taifa Stars).

Semina hiyo inafanyika ukumbi wa Singida Motel, mjini Singida kuanzia kesho (Januari 18 mwaka huu) ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa kwa washiriki kuhusu maboresho hayo.

TFF imeandaa mpango wa maboresho kwa Taifa Stars ambapo pamoja na mambo mengine umepanga kusaka vipaji nchini nzima kwa lengo la kupanua wigo wa kupata wachezaji wanaoweza kuchezea timu hiyo.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager mwaka huu inakabiliwa na mechi za mchujo za Kombe la Afrika (AFCON) ambalo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Morocco.

Mechi hizo za mchujo zitachezwa kati ya Septemba na Novemba mwaka huu ili kupata timu 16 zitakazofuzu kucheza fainali hizo.

SEMINA YA KUPANDISHA MADARAJA WAAMUZI JAN 21
Semina kwa ajili ya kupandisha madaraja waamuzi itafanyika Januari 21 na 22 mwaka huu katika vituo vitatu vya Dodoma, Mwanza na Songea.

Waamuzi watakaoshiriki katika semina hizo ambazo pia zitahusisha mitihani ya utimamu wa mwili (physical fitness test) watajigharamia wenyewe na wanatakiwa kufika vituoni siku moja kabla. Waamuzi hao ni wa daraja la pili na tatu.

Kituo cha Dodoma kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Pwani, Singida na Tanga. Wakufunzi katika kituo hicho ni Paschal Chiganga, Said Nassoro na Soud Abdi.

Wakufunzi wa kituo cha Mwanza kwa ajili ya waamuzi wa mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora ni Alfred Kishongole, Kanali Issarow Chacha, Saloum Chama na Zahra Mohamed.

Kituo cha Songea ni kwa ajili ya waamuzi kutoka Iringa, Lindi, Mbeya, Mtwara, Njombe, Rukwa na Ruvuma. Wakufunzi katika kituo hicho ni Charles Ndagala, Joseph Mapunda, Riziki Majala na Victor Mwandike.

Waamuzi wote wanatakiwa kwenda katika kituo walichapangiwa. Vilevile wanatakiwa kuwa na barua kutoka kwa makatibu wa Vyama vya Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) wa mikoa yao ikiwatambulisha pamoja na kuonesha madaraja yao. 

Post a Comment

0 Comments