Ticker

6/recent/ticker-posts

TAARIFA TATU ZIKO HAPA:KUHUSU IDADI YA WACHEZAJI WA KIGENI WANAOTAKIWA MSIMU WA 2014/2015,MSIBA WA MWAMUZI WA ZAMANI,PAMOJA NA TAARIFA YA WAJUMBE WA NNE WAPYA WA CECAFA

 Na.Boniface Wambura,IMEWEKWA NOV. 26,2013 SAA 02:28 USIKU
Mkurugenzi wa mashindano,Saad Kawemba akizungumza hii leo
Wakati dirisha dogo la usajili linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia
muda uliowekwa.

Pia tunakumbusha kuwa kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30 maana yake ni kuwa haina nafasi ya kuongeza wachezaji.

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), tunakumbusha kuwa kuanzia msimu ujao 2014/2015 watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.

Kuhusu usajili wa wachezaji kutoka nje mpaka sasa hakuna hata klabu moja imeshaingia kwenye TMS kuomba uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system ya TMS itafunga.

RAMBIRAMBI MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mahano, Kiloyi alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka huu) kutoka na ugonjwa wa fangasi ya ubongo, na marehemu amesafirishwa kwenda kwao Kigoma ambapo atazikwa.

Kiloyi alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988 ambapo alipata beji ya FIFA mwaka 2001 akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka 2009, na hadi anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu, IREFA, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu aiweka mahali pema roho ya marehemu Kiloyi.  


WANNE WASHINDA UCHAGUZI CECAFA
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata wajumbe wapya wa wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya leo (Novemba 26 mwaka huu) hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake Leodegar Tenga na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais wa zamani wa FUFA Lawrence Mulindwa
Rais wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza katika uchaguzi huo ambapo wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.

Mulindwa alipata kura zote 12 na kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10), Abdigaani Saeb Arab wa Somalia (9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Atta, Arab na Gisanura walikuwa wakitetea nafasi zao.

Walioshindwa ni Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor aliyepata kura tano na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya aliyepata kura nne.

Post a Comment

0 Comments