Kocha wa
klabu ya soka ya Manchester United ya Uingereza David Moyes anasema
kuwa klabu yake bado haijatoa kitita chochote cha kumsajili mshambulizi
wa Tottenham Hotspurs Gareth Bale.
Hata hivyo Moyes amesema kuwa hawezi kukataa kabisa ikiwa
Manchester United itasonga mbele na kumpata Bale ambaye kwa sasa
anaelekea kusajiliwa na klabu ya Real Madrid ya Uhispania.
Aidha, Moyes ameongeza kuwa United itaendelea kumsaka mchezaji ambaye
ataisaidia timu yake kufanya vizuri katika ligi kuu ya soka nchini
Uingereza.
Imekuwa ikiripotiwa kuwa tayari Real Madrid imekubali kutoa kitita
cha Pauni Milioni 86 kumsajili Bale kwa kipindi cha miaka sita.
Katika hatua nyingine, kocha wa Chelsea Jose Mourihno baada ya timu
yake kulazimisha sare ya kutofungana na Manchester United katika ligi
kuu ya soka Jumatatu, amesema kuwa matumaini ya kumsajili mshambulizi
wa United Wayne Ronney yameanza kudidimia.
Kocha huyo wa Chelsea sasa anasema kuwa amempa Ronney siku mbili
kuamua ikiwa angependa kuichezea Chelsea au kusalia Manchester United
klabu ambayo anasema Rooney hajapata uungwaji mkono.
Uongozi wa United umeendelea kusisitiza kuwa hautamuuza Wayne Rooney
na tayari Chelsea inasema kuwa ikiwa hali itaendelea kuwa hivyo basi
itabidi wamtafute mshambulizi mwingine.
Baada ya mchuano wa siku ya Jumatatu, Chelsea bado wanaongoza msururu
wa ligi kwa alama 7 , Liverpool ni ya pili kwa alama sita sawa na
Tottenham Hotspurs.
Manchester United inashikilia nafasi ya nne kwa alama nne.
CHANZO. RFI KISWAHILI

0 Comments