Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.DEC 04.2016 SAA 09:00 ALASIRI
Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Vijana wa Tanzania wenye umri wa
chini ya miaka 14, leo Desemba 4, 2016 inaanza kambi
rasmi katika
Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Vijana hao 22, wanaingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa
kimataifa dhidi ya Shelisheli unaotarajiwa kufanyika Desemba 17, mwaka
huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ambao una baraka za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA), umepangwa kufuata taratibu zote za kimataifa ikiwa ni
pamoja na kupigiwa Nyimbo za Taifa kwa timu zote sambamba na kupandisha
Bendera za Mataifa husika.
Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu wa timu ya vijana wenye umri
wa chini ya miaka 14, Oscar Mirambo anayepata ushauri kutoka kwa
Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana, Kim Poulsen kinatarajiwa
kuwa na michezo minne ya kirafiki ya nyumbani kabla ya kucheza na
Shelisheli.
Michezo hiyo ya kirafiki ni dhidi ya Moro Kids ya Morogoro Desemba 8,
2016 saa 10.00 jioni kabla ya mchezo wa marudiano Desemba 9, mwaka huu
saa 3.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Jamhuri na baadaye timu hiyo itarejea
Dar es Salaam mchana kujiandaa na safari ya Zanzibar Desemba 11 ambako
itakuwa na michezo miwili mingine ya kirafiki.
Zanzibar itacheza na Kombaini ya timu ya Vijana wa Zanzibar Desemba
12, 2016 kabla ya kurudiana Desemba 14, mwaka huu na timu hiyo na
Kombaini kabla ya kurejea Bara Desemba 15, kujiandaa na mchezo kirafiki
wa kimataifa dhidi ya Shelisheli.
Kikosi kamili cha timu hiyo makipa ni Shaban Hassan Kimwaga na
Abdulatif Noor Lema wakati walinzi ni Kareem Bakari Mfaume, Asante Hamis
Bwatam, Rashid Hamisi Rashid, Moris Michael Njako, Harubu Juma Tanu,
Cosmas Lucas Jakomanya, Salim Abubakar Lupepo na Dastan Daniel Matheo.
Viungo ni Edson Jeremiah Mshirakandi, Jonathan Raphael Kombo,
Alphonce Mabula Msanga, Erick Boniface Bunyaga, Gssper Godfrey
Gombanila, Sabri Dahari Kondo na washambuliaji ni Jafari Juma Rashid,
Ludaki Juma Chasambi, Steven Emmanuel Sodike, Michael Mussa Mpubusa na
Edmund Geofray John.
Timu hii inaundwa na vijana ambao TFF iliwakusanya tangu 2014 na
kuwaunganisha kwa pamoja katika Shule ya Msingi na Sekondari ya Kukuza
Vipaji ya Alliance iliyoko Mwanza. Mbali ya kutoa elimu ya msingi na
sekondari, pia Alliance inatoa elimu ya awali kwa watoto wa kuanzia umri
wa miaka miwili hadi sita.
Timu hii inaandaliwa kuja kwa time mpya ya Vijana wenye umri wa chini
ya miaka 17 ambao watashiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa
vijana mwaka 2019 ambako Tanzania imeteuliwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) kuwa mwenyeji. Kambi itavunjwa Desemba 18, mwaka huu.
0 Comments