Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.DEC 02.2016 SAA 12:59 JIONI
Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Gianni
Infantino bado ameguswa na vifo vya wachezaji wa timu ya soka
Chapecoense Real ya Brazil vilivyotokea Jumatatu.
Rais Infantino ameagiza timu zote duniani kuendeleza utaratibu wa
kuwaombea dua kabla ya mchezo kwa mechi zote zinazopigwa mwishoni mwa
juma hili kuanzia leo Ijumaa ambao Tanzania kutakuwa na mchezo wa Ligi
ya Vijana katika vituo vya Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.
Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Brazil (CBF), Lucca Victorelli
kutokana na vifo hivyo vilivyotokana na ajali iliyoua zaidi ya watu 76
kati ya 81 waliokuwa kwenye ndege moja.
Kwa upande wake, Rais Infantino ametuma waraka kwa kila Shirikisho au
Chama cha Mpira wa Miguu Duniani akisema kwamba utamaduni wa kusimama
kwa dakika moja uendelezwe kwa kila mchezo utakaochezwa kuanza leo
Ijumaa hadi Jumatatu.
Ishara za maombolezo hayo, ziende sambamba na kufunga kitambaa cheusi
mkononi ili kuwakumbuka wachezaji hao, wanahabari kadhalika abiria
wengine ambao kwa pamoja walikuwa kwenye ajali hiyo iliyonusurisha watu
watano tu.
Ndege hiyo iliyotumiewa na wacheaji hao wakiwamo abiria wengine
ilikuwa ikisafiri Jumatatu kutoka Brazil kupitia Bolivia kwenda Colombia
kwenda kucheza mechi ya fainali ya michuano ya ubingwa wa Kombe la
Amerika ya Kusini (Copa Sud Americana).
Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini,
iliyotarajiwa kuchezwa Jumatano Novemba 30, 2016 ambako Chapecoense
Real ingecheza dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba wachezaji wa timu ya Chapecoense Real ya
Brazil na awali ilitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na
hitilafu kwenye mfumo wa umeme, na hatimaye kuanguka muda mfupi baadaye
karibu na mji wa Medelin.
Wachezaji walionusurika wanatajwa kuwa ni Alan Ruschel, golikipa
Danilo na Jackson Follmann na kwamba walipatiwa huduma ya kwanza katika
hospitali iliyoko katika mji wa Le Ceja nchini Colombia.
0 Comments