Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.NOV 11.2016 SAA 01:34 USIKU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za
kifo cha
Mbunge wa Jimbo la Dimani Fumba, Zanzibar, Mheshimiwa Hafidh
Tahir Ali aliyefariki dunia kwenye Hospitali Kuu ya Dodoma usiku wa
kuamkia leo Novemba 11, 2016.
TFF ilijulishwa kifo cha Mheshimiwa Hafidh na
Mbunge wa Jimbo jipya la Ulyankulu, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, John
Kadutu ambaye alisema leo walikuwa na programu ya kusafiri kwenda
Tabora kushiriki mazishi ya Mbunge wa zamani wa Urambo, Samwel Sitta
lakini kabla ya kwenda mazoezi alfajiri, waliarifiwa kuhusu kifo hicho.
“Inasikitisha, lakini ni ya Mungu yote,” alisema Kadutu.
Kifo hicho kimemsikitisha Rais Malinzi ambaye
alituma salamu za pole na rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akisema taifa limepata msiba mwingine
mzito kwa Mwamuzi wa zamani wa kimataifa wa mpira wa miguu aliyekuwa
anatambuliwa/kuwa na beji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA).
Hakika alikuwa kiongozi wa karibu na watu hasa
kutokana na michezo ambayo siku zote alikuwa akiota ndoto za kuifikisha
mbali hasa ukirejea kuwa ni jana tu Novemba 10, mwaka huu alichaguliwa
na wanachama wenzake wa Young Africans - tawi la Bunge kuwa Katibu wa
tawi hilo chini ya Mwenyekiti Venance Mwamoto – Mbunge wa Kilolo mkoani
Iringa.
Ukaribu huo na watu ndio uliompaisha wakati fulani
kuwa mmoja watangazaji mahiri wa redio alipoganya kazi hiyo na manguli
wengine kama David Wakati kabla ya kuwa Msemaji wa Serikali ya Awamu ya
Tano ya SMZ kabla ya kuwa Mbunge wa RahaLeo.
“Wiki hii imekuwa ngumu kwangu, tumepoteza
viongozi wa mfano na wanamichezo mahiri katika kucheza michezo hususani
mpira wa miguu na kuuongoza hata kama ni kwa mawazo yao chanya tu.
Mheshimiwa Hafidhi ni sehemu ya wanamichezo hao mahiri, ni pigo kubwa
hasa kwenye tasnia ya mpira wa miguu. Dua zetu ni Mwenyezi Mungu
amghufie na kumrehemu marehemu,” alisema Malinzi.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Malinzi pia
alitoa pole kwa familia ya marehemu Hafidh Tahir Ali, ndugu, jamaa,
majirani, na marafiki hususani wapiga kura wa Jimbo la Dimani Fumba kwa
kumpoteza kiongozi wao hivyo kuwataka kuwa watulivu wakati huu mugumu
kwao.
Pia Rais Malinzi amesema vifo cha Sheikh Said
Mlohammed, Mzee Mheshimiwa Sitta na Mheshimiwa Tahir, vibaki kuwa sehemu
ya funzo kwetu katika kujiandaa na maisha ya baadaye kwa sababu zote ni
wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
Inna lillah wainn ilayh Rajiuun.
0 Comments