Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.SEPT.09,2016 SAA 12:00 JIONI
Baada ya jana Septemba 8, 2016 kuilaza Burundi kwenye mchezo wa
kirafiki wa kimataifa, Timu ya Mpira wa Miguu ya Taifa ya
wanawake wa
Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’, inatarajiwa kuondoka leo kwenda
Jinja, Uganda kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) maarufu kama Kombe la CECAFA
itafanyika kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016.
Burundi pia inakwenda Uganda ambako imepangwa makundi tofauti katika
michuano hiyo. Tanzania kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na
Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar
pamoja na mwenyeji Uganda,.
Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12,
2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia
zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa
kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.
Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya
zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza
na Uganda. Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga
hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.
Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika
Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na
nne.
Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya
kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka
la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa
kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani
kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa
safari ya Uganda.
0 Comments