Kocha Mkuu wa timu ya soka ya
vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ya Shelisheli, Gavan Jeanne ameonesha
kuihofia
Serengeti Boys ya Tanzania katika mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza
fainali za Kombe la Mataifa utakaofanyika Juni 26, 2016 kuanzia saa 10.00 jioni
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Jeanne alionesha hofu hiyo leo
Juni 25, 2016 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na mbele ya Kocha
Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime ambao kwa pamoja walikuwa wakmizungumzia
namna walivyoandaa timu zao kwa ajili ya mchezo huo wa kesho.
“Hatujawahi kushiriki michuano ya
vijana. Hii ni mara yetu ya kwanza. Tumekuja kujifunza kwa wenzetu Tanzania
ambao wana uzoefu,” alisema Jeanne ambaye pia alithibitisha kuwa hawajawahi
kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa.
Kwa upande wa Bakari Shime wa
Serengeti Boys, alisema ameindaa mechi hiyo vema kiakili na kimwili kwa ajili
ya kuikabili Shelisheli katika mchezo huo ambao hamasa yake imekuwa kubwa kwa kuwa
kikosi hicho kinaandaliwa kuwa timu ya taifa baada ya miaka miwili.
Wachezaji wa Serengeti Boys
wamesema, watafanya vema kwenye mchezo huo. Wachezaji hao ni Anthony Shilole
ambaye alisema: “Tumejifunza mambo mengi, ushindi ni lazima kwa sababu
tutafuata maelekezo ya walimu wetu. Tutajitahidi tushinde.”
Ally Ng’anzi: Maandalizi ni
mazuri. Mechi ya Jumapili tumejiandaa vema. Tunashinda tena kwa magoli mengi.”
Ally Msengi: “Watanzania
watarajie ushindi baada ya maandalizi ya muda mrefu. Timu iko kambini kitambo.”
Kennedy Nashony: Tutapambana
kadiri ya uwezo. Kila mechi kwetu ni fainali. Hatuko tayari kupoteza ili kukosa
mechi zijazo.”
Shelisheli ilitua Ijumaa usiku
saa 7.45 usiku ikiwa na viongozi 25 na imefikia hoteli ya Southern Sun iliyoko
katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Waamuzi wanne kutoka Ethiopia,
ndio watakaochezesha mchezo huo. Waamuzi hao ni Belay Tadesse Asserese ambaye
ni mwamuzi wa kati wakati wasaidizi wake ni Tigle Gizaw Belachew upande wa
kulia na Kinfe Yilma Kinfe upande wa kushoto huku mwamuzi wa akiba atakuwa
Lemma Nigussie. Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Bester Kalombo.
Serengeti Boys ilikuwa kambini
tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mchezo huo wa kufuzu fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika dhidi ya vijana wenzao wa Shelisheli utakaofanyika Juni 26,
mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Mchezo wa marudiano
kati ya Serengeti Boys na Shelisheli utachezwa Julai 2, 2016 huko Shelisheli.
Katika kuajindaa na mchezo huo,
Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya
Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016)
kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi
za Afrika Mashariki.
0 Comments