Ofisa Habari wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire |
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa adhabu kwa watu tisa wakiwemo
viongozi, wachezaji na kocha mmoja kwa kupatikana na hatia ya makosa ya kinidhamu.
Katika kikao chake kilichofanyika juzi (Februari 3 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Kamati hiyo imewafungia mwaka mmoja viongozi wawili wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) Mkoa wa Mwanza kwa kuwashawishi wachezaji wa Mwanza Queens kugomea uamuzi halali.
KUTOKA KULIA:Ofisa habari wa TFF Baraka Kizuguto, mkurugenzi wa mashindano wa Tff Boniface Wambura na katibu mkuu wa TFF Selestine Mwasingwa,wakizungumza hii leo. |
Sophia Tigalyoma (Mwenyekiti) na Katibu wake Hawa Bajanguo walitiwa hatiani kwa kuwashawishi wachezaji kugomea uamuzi wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF kutupa rufani yao dhidi ya Kigoma.
Kocha wa Polisi Tabora, Eliakim Christopher amefungiwa mechi kumi na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 39(2) ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kutiwa hatiani kwa kumtukana refa wakati wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa mjini Moshi.
Wachezaji wa JKT Oljoro FC, Dihe Makonga, Swaleh Idd Hussein, Ramadhan Mnyambegu na nahodha Shaibu Nayopa wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kuzingatia kanuni ya 36(10) ya FDL kutokana na kufanya vurugu kwenye mechi kati yao na Burkina Faso iliyochezwa mjini Morogoro.
Mtunza Vifaa (Kit Man) wa JKT Oljoro FC, Eliud Mjarifu amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi kati ya timu hizo iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Pia Mjarifu amepewa onyo kali na kutakiwa kutorudia tena kutenda kosa, kwani hata mwenendo wake wakati wa shauri hilo ulionyesha utovu wa nidhamu mbele ya Kamati.
Naye Mtunza Vifaa wa Rhino Rangers FC, Albert Mbuji amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 200,000 kwa kupatikana na hatia ya kuwatukana na kugomea uamuzi wa marefa kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma. Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 40(2) ya FDL.
Kamati hiyo imeondoa malalamiko dhidi ya Ofisa Habari wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire kwa vile refa Israel Mujuni Nkongo ambaye ni mlalamikaji hakufika kwenye shauri hilo.
Nkongo alimlalamikia Bwire akidai alitoa maneno yenye kuweza kuchochea chuki dhidi yake kwa waamuzi, kwani kupitia redio 100.5 Times FM, Bwire alidai refa huyo ndiye aliyeshinikiza kuondolewa kwa refa Mohamed Theofil kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Pia Kamati hiyo imemkuta bila hatia Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda ambaye TFF ilimlalamikia kuwa akiwa mtendaji mkuu wa chama hicho alishindwa kuhakikisha timu ya Singida inaingia uwanjani kucheza na Dodoma kwenye mechi ya Kombe la Taifa kwa Wanawake.
Kamati ilikubaliana na utetezi wa Gunda kuwa, jukumu la timu hiyo lilikuwa mikononi mwa viongozi wa TWFA Singida, na tayari SIREFA kupitia Kamati yake ya Nidhamu ilishatoa adhabu kwa viongozi wa timu hiyo kutokana na kitendo hicho.
Nayo malalamiko ya Polisi Tabora FC kutaka mechi yao dhidi ya Toto Africans FC irudiwe kwenye uwanja huru (neutral ground) kwa madai ya kuchezeshwa zaidi ya muda unaotakiwa, na kutokuwepo ulinzi wa kutosha kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza yamekataliwa.
Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu za Mwadui FC na Polisi Mara FC dhidi ya Toto Africans kwa kumchezesha mchezaji Ladislaus Mbogo bila kuonyesha leseni yake yasikilizwe haraka na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa vile si ya kinidhamu.
Wakati huo huo, Kamati ya Nidhamu inaendelea na kikao chake leo (Februari 5 mwaka huu) kusikiliza malalamiko mengine ya kinidhamu yaliyofikishwa mbele yake.
TFF YAONYA KUHUSU UENDESHAJI MPIRA WA MIGUU
Kutokana na matatizo mbalimbali ya kiutendaji yaliyojitokeza kwenye uendeshaji, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa hadhari kuwa shughuli zote za mpira wa miguu zinazohusu mkoa wowote wa Tanzania Bara zitasimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa husika, yakiwemo mashindano ya Kombe la Taifa la Wanawake.
KWA TAARIFA,BREAKING NEWS,RATIBA PAMOJA NA MATOKEO YA MECHI MBALIMBALI,LIKE PAGE YA FACEBOOK BONYEZA HAPA (Jamii na Michezo) .
0 Comments