Mhariri:Herman Kihwili.IMEWEKWA DESEMBA 29.2013 SAA 07:30 USIKU
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo
mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo
ambapo klabu zenye matatizo
zimepewa hadi Januari 10 mwakani
kurekebisha.
Baadhi
ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa
hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati
yenyewe.
Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.
Pia
klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au
kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati
imeshawaondoa katika orodha yao.
RAGE BADO MWENYEKITI HALALI SIMBA
Ismail
Aden Rage ndiye Mwenyekiti halali wa Simba ambapo Kamati ya Sheria na
Hadhi za Wachezaji imemtaka kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa taratibu
za klabu ya Simba.
Kamati
imebaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya
Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha
Mwenyekiti wao. Upungufu huo ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya
Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha
Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.
Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.
Hivyo,
agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe
mkutano lipo palepale. Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa
kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.
Katika
mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya
Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa
na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya
Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.
TFF
inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na
klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji
wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.
Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.
Kuhusu
mchezaji Emmanuel Okwi ambaye aliuzwa nchini Tunisia, TFF inafahamu
kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa na itasaidia kufuatilia FIFA fedha
za mauzo ya mchezaji huyo.
AJENDA, MUHTASARI WA KUMNG’OA KATIBU COREFA ZATAKIWA
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao
vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.
Ajenda
na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji
iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na
Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.
WATAKIWA KUHESHIMU UAMUZI WA TPLB
Wanachama
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wametakiwa kuheshimu
uamuzi halali unaofanywa na vyombo vyake kwa kuzingatia katiba na kanuni
zake.
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imetoa maelekezo hayo baada ya
klabu ya Stand United kukata rufani kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu
Tanzania (TPLB) kuagiza mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi
ya Kanembwa JKT iliyovunjika kurudiwa Februari Mosi mwakani mjini
Tabora.
Sekretarieti
ya TFF iliwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ili itoe mwongozo kwa vile uamuzi huo uliofanywa na TPLB
hauwezi kukatiwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za ligi husika.
Kamati
imesisitiza kuwa hiyo ni falsafa ya mpira wa miguu ambapo uamuzi
unaofanywa uwanjani haukatiwi rufani, hivyo uheshimiwe kama ilivyo kwa
masuala ya mpira wa miguu kutopelekwa katika mahakama za kawaida za
kisheria.
PAN AFRICAN WATAKIWA KUFUATA NGAZI HUSIKA
Wanachama wa Pan African wametakiwa kufuata ngazi husika pale wanapoona viongozi wa klabu yao wanakwenda kinyume na Katiba yao.
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imetoa mwongozo huo kwa wanachama wa
Pan African baada ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulalamikia uongozi wao wakati wao si
wanachama wa TFF.
Wanachama
hao wanalalamikia uongozi wa klabu yao kwa kuitisha mkutano wa uchaguzi
kabla ya ule wa kawaida ambao unatakiwa kufanyika mara moja kwa mwaka.
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imelazimika kutoa mwongozo huo
kwa vile wanachama hao katika malalamiko yao wamekigusa Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ambacho ni mwanachama wa TFF.
Pan
African ni mwanachama wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala
(IDFA) ambao ndiyo wanachama wa DRFA. Hivyo, TFF imemtaka mwanachama
wake DRFA kupitia IDFA kufuatilia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.
0 Comments