Ticker

6/recent/ticker-posts

MWISHO WAKO LINI KUINGIA MAKTIBA?,BASI TAARIFA HII INAKUHUSU

Na.Jackline Mshana ,IMEWEKWA DISSEMBA 3,2013 SAA 09:45 MCHANA

Jackline Mshana akizungumza leo hii
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (iliyokuwa ikijulikana kama Bodi ya Huduma za Maktaba
Tanganyika), ni shirika la umma lililopo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Shirika hili lilianzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 39 ya mwaka 1963 likijulikana kama Bodi ya Huduma za Maktaba Tanganyika. Huduma kwa umma zilianza kutolewa rasmi tarehe 01 Aprili, 1964.
Mwaka 1975, sheria ya mwaka 1963 ilirekebishwa ambapo sheria mpya ya Bunge Namba 6 ya mwaka 1975 iliundwa na kupelekea jina la shirika kubadilika kutoka Bodi ya Huduma za Maktaba Tanganyika na kuwa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMATA).
Lengo kuu la kuundwa kwa BOHUMATA lilikuwa kutoa fursa kwa wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote kutumia Maktaba za umma ili kujipatia elimu, maarifa, taarifa mbalimbali zitakazowasaidia katika kujikwamua kutoka katika umaskini na ujinga na pia kupata burudani na kudumisha utamaduni.
MAJUKUMU YA BODI
Majukumu ya msingi ya Bodi yanatekeleza mahitaji ya sheria ya Bunge Namba 6 ya mwaka 1975. Majukumu hayo ni:

·                Kuanzisha, kuendesha, kuongoza, kuboresha, kutunza na kuendeleza Maktaba za umma kote nchini kuanzia ngazi ya Mikoa, Wilaya hadi Tarafa.

·                Kuupatia umma wa Watanzania taarifa mbalimbali zilizokusanywa kutoka katika ulimwengu mpana wa maarifa kwa ajili ya elimu, utafiti na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.

·                Kukusanya na kuhifadhi machapisho ya kitaifa.

·                Kutoa mafunzo na kuendesha mitihani ya taaluma ya Ukutubi kwa wafanyakazi wa Bodi, Maktaba za shule, Vyuo na Taasisi mbalimbali nchini.

·                Kutoa ushauri na uelekezi kwa Idara za Serikali, Taasisi na Mashirika mengine kuhusu kuanzisha, kuendeleza na kuboresha huduma za Maktaba katika maeneo yao.

·                Kuendeleza mfumo wa ushirikiano kati ya Maktaba za BOHUMATA na Taasisi nyingine zinazotunza nyaraka ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa kwa urahisi.

MTANDAO WA HUDUMA
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania inatoa huduma katika mikoa 22, wilaya 19 na tarafa 2, kutoka Maktaba 3 zilizokuwepo wakati ilipoanza kutoa huduma kwa umma mwaka 1964.

Dira ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania ni kuwa Taasisi ya umma inayoongoza nchini katika kutoa na kusambaza taarifa mbalimbali kwa njia ya vitabu, machapisho na teknolojia ya kisasa kupitia mtandao wa maktaba zake kote nchini.
Dhima ya BOHUMATA ni kutoa na kusambaza huduma sahihi kwa watu wote kwa wakati muafaka ili kuendeleza kisomo, kujiburudisha na kuendeleza utamaduni kwa jamii. Pia kukusanya, kutayarisha na kuhifadhi machapisho kwa matumizi ya kizazi kijacho.
MAFANIKIO KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2012/2013

1).   Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania iliwezesha kupatikana kwa jumla ya vitabu 25,516; kati ya hivyo, 468 vilipatikana kwa mujibu wa sheria Na. 6 ya Mwaka 1975, vitabu 24,984 vilipatikana kwa njia ya msaada na vitabu 64 vilinunuliwa na hivyo kufanya idadi ya vitabu vyote katika Maktaba nchini kufikia 1,210,473.
2).   Ilitoa ushauri kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa Maktaba katika shule 22 na taasisi 7.
3). Ilipokea jumla ya watumiaji wa Maktaba 1,199,243 ambapo kati yao 999,243 walikuwa wa  muda mfupi na 200,000  wa muda mrefu.
4).   Ilianzisha miradi miwili yenye lengo la kuipatia jamii habari kwa kutumia TEHAMA kwa kushirikiana na Chama cha Ukutubi cha Ufini (Finnish Library Association) na Taasisi ya Electronic Information for Public Libraries ya nchini Ujerumani) ambapo makundi yafuatayo yalinufaika: wakulima, wafugaji, vijana na wajasiriamali.
5).   Iliwezesha udahili wa wanafunzi 1,196 wa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS), Bagamoyo; ambapo ngazi ya Cheti walikuwa 502, Stashahada 545 na wa mafunzo ya muda mfupi 149.
6).   Ilikamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike, yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 64 katika Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS), Bagamoyo.
7). Ilifanya mkutano mkubwa ujulikanao kama Maktaba kwa Maendeleo uliokuwa na lengo la kutambua / kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa Maktaba katika Jamii, ambao ulikutanisha zaidi ya wadau 300 kutoka Tanzania, Kenya, Namibia, Ujerumani, Ufini, na Uingereza.

CHANGAMOTO
Uhaba wa fedha za maendeleo na za matumizi mengineyo ambao unapunguza kasi ya: kuendeleza na kukarabati miundo mbinu ya Maktaba, ununuzi wa vitabu, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA, uendelezaji wa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS), Bagamoyo na kuwaendeleza watumishi kielimu.
BOHUMATA imekuwa ikifanya yafuatayo ili kukabiliana na changamoto hizo:
1). Kuandaa maandiko mradi  mbalimbali ya kuombea misaada kwa wafadhili.
2).  Kushirikiana na Halmashauri za wilaya kuendeleza huduma za Maktaba wilayani.
3). Kuendeleza ushirikiano na mashirika mbalimbali kama vile ‘Book Aid International’ la nchini Uingereza na ‘Children International’ la nchini Marekani, UNESCO - Tanzania wanaoipatia BOHUMATA misaada ya vitabu na vifaa vya TEHAMA.
4). Kuwajengea uwezo watumishi wa vituo vya Bodi ili waweze kutafuta wafadhili wa kuviendeleza vituo hivyo.

MIPANGO IJAYO
1).  BOHUMATA ina mpango wa kuboresha zaidi huduma za Maktaba kwa jamii kwa kutumia TEHAMA kwa kutumia Katalogi ya Kielektroniki. Hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni kununuliwa kwa ‘server’ na vifaa vingine husika, kuanza programu ya mafunzo kwa watumishi na inakadiriwa kuwa mpaka kufikia mwezi Machi Mwaka 2014 BOHUMATA itaanza kutumia Katalogi ya Kielektroniki kwa kuanzia Maktaba Kuu ya Taifa – Dar es Salaam ndiyo itakayohusika na vituo vingine vitafuata.
2).  Itakapofika tarehe 01 Aprili, 2014 BOHUMATA itafanya maadhimisho ya miaka hamsini (50) tangu ilipoanza kutoa huduma za Maktaba kwa jamii hivyo umma unafahamishwa kushiriki ambapo baadhi ya mambo yatakayojiri ni pamoja semina/ kongamano, mahema ya usomaji na kutangaza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 kwa vyombo vya habari.
HITIMISHO
BOHUMATA inawashukuru wadau mbalimbali kwa ushirikiano uliopo katika kusaidia kutekeleza malengo yake ikiwemo wizara mama; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania, UNESCO – Tanzania,  Ubalozi wa China – nchini Tanzania, Chama cha Ukutubi cha Ufini, na taasisi ya Electronic Information for Public Libraries (EIFL).
Maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni yanategemea kupatikana kwa taarifa sahihi na kwa wakati unaofaa. Hivyo Watanzania wanashauriwa kutumia Maktaba na rasilimali habari zilizopo ili kuwawezesha kumudu maisha yao kulingana na fani mbalimbali za maisha.






BODI YA HUDUMA ZA MAKTABA TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

A: TAARIFA YA KIPEKEE
1).   BOHUMATA kwa msaada wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imefanikiwa kutanua huduma za Maktaba karibu zaidi na wananchi ambapo imefikisha huduma hizo katika mikoa 22 na wilaya 19. Kwa ngazi ya mikoa mafanikio ni makubwa na katika wilaya juhudi zilizopo kulingana na Mpango Mkakati wa Shirika wa mwaka 2008/2009 – 2018/2019 ni kushirikiana na Halmashauri za Wilaya nchini ili kuanzisha huduma za Maktaba wilayani ambapo  mafanikio hayo yamepatikana katika wilaya za Ruangwa, Chunya, Masasi, Mbulu na Ngara.
2).  Upanuzi wa Chuo cha Ukutubi na Uhifanyi wa Nyaraka (SLADS), Bagamoyo ambapo udahili wa wanafunzi umeongozeka kutoka wanafunzi 100 mwaka 2007 na kufikia wanafunzi 1,093 mwaka 2013. Chuo hiki kinatoa mchango mkubwa wa upatikanaji wa wakutubi kulingana na ongezeko la Maktaba katika taasisi mbalimbali nchini.
3).     Kusaidia kuinua kiwango cha elimu kwa kusambaza vitabu vya msaada kwa shule nchini hasa katika mikoa ya pembezoni na pia katika taasisi mbalimbali. 
3).  Kutoa huduma za Maktaba kwa jamii kwa kutumia TEHAMA kwa kuwafikia wahusika walipo. Kupitia miradi miwili iliyofadhiliwa  na Chama cha Ukutubi cha Ufini (Finnish Library Association) na Taasisi ya Electronic Information for Public Libraries ya nchini Ujerumani) na kutekelezwa Dar es Salaam na Morogoro ambapo makundi yafuatayo yananufaika: wakulima, wafugaji, vijana na wajasiriamali.
4).    BOHUMATA ina mpango wa kuboresha zaidi huduma za Maktaba kwa jamii kwa kutumia TEHAMA kwa kutumia Katalogi ya Kielektroniki. Hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni kununuliwa kwa ‘server’ na vifaa vingine husika, kuanza programu ya mafunzo kwa watumishi na inakadiriwa kuwa mpaka kufikia mwezi Machi Mwaka 2014 BOHUMATA itaanza kutumia Katalogi ya Kielektroniki kwa kuanzia Maktaba Kuu ya Taifa – Dar es Salaam ndiyo itakayohusika na vituo vingine vitafuata hivyo siku za usoni BOHUMATA itakuwa ya kisasa zaidi. Pia katika Chuo cha Ukutubi ipo maabara ya kompyuta.
5).  Itakapofika tarehe 01 Aprili, 2014 BOHUMATA itafanya maadhimisho ya miaka hamsini (50) tangu ilipoanza kutoa huduma za Maktaba kwa jamii hivyo umma unafahamishwa kushiriki ambapo baadhi ya mambo yatakayojiri ni pamoja semina/ kongamano, mahema ya usomaji na kutangaza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 kwa vyombo vya habari.

B: HITIMISHO
v    BOHUMATA inawashukuru wadau mbalimbali kwa ushirikiano uliopo katika kusaidia kutekeleza malengo yake ikiwemo wizara mama; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania, UNESCO – Tanzania,  Ubalozi wa China – nchini Tanzania, Chama cha Ukutubi cha Ufini, na taasisi ya Electronic Information for Public Libraries (EIFL).
v    Maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni yanategemea kupatikana kwa taarifa sahihi na kwa wakati unaofaa. Hivyo Watanzania wanashauriwa kutumia Maktaba na rasilimali habari zilizopo ili kuwawezesha kumudu maisha yao kulingana na fani mbalimbali za maisha.

Post a Comment

0 Comments