Na.Boniface Wambura,IMEWEKWA DISEMBA 8,2013 SAA 01:26 USIKU
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa
changamoto kwa uongozi mpya wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kusukuma mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini.
Ametoa
changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar
Tenga na kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila
utakapohitajika katika shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira
wa miguu Tanzania.
Rais
Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa
ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye
binafsi (Rais Kikwete) na Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa
katika kuendeleza mpira wa miguu nchini.
“Pongezi
zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha
kiwango cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
“Kwa
niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati
kwako wewe na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu muhimu
mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu nchini.
“Mafanikio
ya kutia moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete
katika barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli
zake.
Hata
hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo inapataka,
lakini dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni
uongozi mpya kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu
nchini.
Tenga
ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa
Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi
viwili kuanzia Desemba 2004 hadi Oktoba 2013.
0 Comments