Na.Boniface Wambura,IMEWEKWA NOV. 30,2013 SAA 03:00 USIKU
SALAMU ZA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA KWENYE HAFLA YA
KUPOKEA KOMBE HALISI LA DUNIA TANZANIA
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dk. Fennela Mukangara- Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Ndugu Dioniz Malinzi- Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
Mkuu wa msafara wa FIFA/Coca cola
Bw Yebeltal Getachew- Meneja Mkazi wa Cocacola
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na mabwana
Mheshimiwa
Rais, nianze kwa kukushukuru kwa heshima uliyoupatia mpira wa Tanzania
kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla yetu hii ya kupokea Kombe
halisi la Dunia.
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kupewa heshima hii na FIFA na washirika wake kampuni ya vinywaji ya Coca-Cola.
Coca-Cola ni washirika wetu wa karibu na wamekuwa
wakidhamini mashindano ya kitaifa ya vijana tangu
mwaka
2007, mashindano ambayo kwa kiasi kikubwa yamesaidia kuibua vipaji
vingi ambapo baadhi yao wameweza kuchezea timu zetu za Taifa na klabu za
Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.
Tunawashukuru sana Coca-Cola na tunaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao za
kuendeleza soka ya vijana.
Mheshimiwa Rais, tarehe 19 Novemba, 2009 wakati
unapokea kombe hili hili hapa Tanzania ulitoa changamoto kadhaa kwa uongozi wa mpira wa Tanzania.
Ulitushauri
tuimarishe uongozi na utendaji wetu kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa,
Wilaya hadi klabu, ulitushauri tupate walimu wenye uzoefu wa kutosha
kufundisha timu zetu za mpira na pia ulitushauri tuwekeze katika kuibua
na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka wakiwa na umri mdogo.
Mheshimiwa Rais ushauri wako kwetu tuliuzingatia na
tulifanya jitihada za kuufanyia kazi.
Hali
ya utulivu katika uendeshaji mpira wetu imeimarishwa na pale
palipoonyesha dalili za migogoro tulikemea na ikibidi tulichukua hatua
madhubuti kutatua migogoro.
Tumefanya kozi mbalimbali za kuwaendeleza walimu wetu wa mpira,
waamuzi, madaktari na viongozi wetu wa ngazi mbalimbali na matokeo yake
yanaonekana katika kuinuka kwa viwango vyao vya ufundishaji na utoaji
uamuzi uwanjani.
Mheshimiwa Rais kama ulivyotuelekeza mwaka 2009
maendeleo
ya soka ya vijana ndio ufunguo wa maendeleo ya mpira kwa Taifa letu.
Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe 28, Oktoba
2013 tayari unalifanyia kazi jambo hili kwa umakini mkubwa.
Uongozi
wetu umeamua kuwa ufunguo wa mpango endelevu wa soka ya vijana utakuwa
ni Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika za vijana chini ya umri
wa miaka 17 mwaka 2019.
Fainali hizi uhusisha mataifa manane yanayogawanywa
Katika makundi mawili ya awali akiwemo mwenyeji
ambaye
anaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya fainali hizi. Aidha
timu mbili zinazoongoza makundi haya mawili moja kwa moja huwa zinacheza
fainali za dunia za vijana chini ya umri wa miaka
17.
Fainali
hizi ndizo ziliwaibua akina Luis Figo, Ronaldino, Nwankwo Kanu, Michael
Essien, Nii Lamptey, Celestine Babayaro na wengine kadhaa.
Ili tupate timu nzuri ya vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 itabidi mwaka kesho 2014 tufanye
mashindano ya kitaifa
ya vijana chini ya umri wa chini wa miaka 12 ili tupate kikosi cha
kwanza cha Taifa U-12, kikosi ambacho kitakuwa pamoja kuelekea 2019.
Katika
kuboresha kikosi hiki mwaka 2015 tutafanya mashindano ya kitaifa ya
umri chini ya miaka 13, 2016 yatakuwa ya umri chini ya miaka 14, 2017
yatakuwa ya umri chini ya miaka 15 na 2018 yatakuwa ya umri chini ya
miaka 16 na ambayo yatatupatia kikosi cha mwisho cha kuingia nacho
fainali za vijana mwaka 2019.
Tunaamini timu nzuri za Taifa U-17 ya mwaka 2019
itatuzalishia kikosi imara kitakachoshiriki Olimpiki za 2020, kucheza CHAN na AFCON zitakazofuata
na hatimae kufaulu fainali za dunia 2026 ambayo ni miaka kumi na tatu kuanzia sasa.
Ninashukuru
tarehe 21 Novemba 2013, Shirikisho la mpira barani Afrika (CAF)
liliniteua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Afrika
umri
chini
ya miaka 17 (CAF U-17 Organizing Committee), tunaamini kuwepo kwangu
katika kamati hii muhimu ya CAF kutasaidia Tanzania ipate wenyeji huu
mwaka 2019.
Mheshimiwa
Rais kwa mujibu wa kanuni za CAF nchi inayoomba uenyeji wa fainali za
michuano ya Afrika haina budi ionyeshe barua ya kuungwa mkono na nchi
yake(Letter of support from Government).
Wiki
ijayo tutawasilisha barua kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo ya kuomba kuungwa mkono na Serikali katika azma yetu hii,
tunaomba Serikali ituunge mkono katika jambo hili.
Mheshimiwa Rais nimalizie kwa kukushukuru tena kwa
uwepo wako katika shughuli hii muhimu, ninaishukuru
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa
ushirikiano
wanaotupa katika shughuli zetu za kila siku, FIFA nawashukuru sana kwa
kutuwezesha kuwa moja ya nchi 88 duniani zilizopokea kombe hili,
Coca-Cola asanteni sana tuzidi kuwa karibu.
Watanzania wenzangu ninaomba tuje kwa wingi
kesho Jumamosi kutembelea Uwanja wa Taifa,
Dar
es Salaam na kuliona Kombe hili na kupiga nalo picha. Imani yangu ni
kuwa ipo siku Kapteni wa Timu yetu ya Taifa atamkabidhi Rais wa Tanzania
kombe hili.
Asante
0 Comments