IMEWEKWA NOVEMBA 1,2013 SAA 12:35 JIONI
KUFUATIA matukio yaliyotokea
katika pambano la jana, Alhamisi, Oktoba 31, 2013 dhidi ya Kagera Sugar kwenye
Ligi Kuu ya
Tanzania, klabu ya Simba inapenda kutoa maelezo yafuatayo.
Mosi, Simba SC inalalamikia
uchezeshaji mbovu wa mwamuzi, Mohamed Theofilo kutoka mkoani Morogoro ambaye
ndiye aliyekuwa mwamuzi wa kati katika mechi ya jana.
Kwa bahati nzuri, baadhi ya
vyombo vya habari vya hapa nchini tayari vimeandika kwamba mwamuzi huyo
hakumudu mchezo wa jana na hivyo maelezo haya ya klabu hayatokani na uchungu wa
kupoteza pointi mbili muhimu bali ni ukweli wa wazi.
Mara zote klabu ya Simba
imekuwa ikisisitiza umuhimu wa waamuzi kufuata Sheria zote 17 zinazotawala
mchezo huu. Katika pambano la jana, adhabu ya penalti aliyoitoa mwamuzi haikuwa
halali na ilitolewa katika wakati ambapo muda wa kuchezwa mechi hiyo ulikuwa
umemalizika.
Mchezaji aliyedaiwa kufanyiwa
madhambi aliushika mpira akiwa nje ya eneo la penalti na alijirusha mwenyewe (diving)
kwenda kwenye eneo la hatari. Mwamuzi msaidizi ambaye alikuwa jirani na tukio
hakuonyesha bendera kuashiria madhambi yoyote yaliyofanyika lakini cha ajabu,
Theofilo ambaye alikuwa umbali wa zaidi ya mita 30 kutoka eneo la tukio, ndiye
aliyeona madhambi na kuamuru penalti.
Penalti hiyo ilitolewa katika
dakika ya tano na nusu wakati muda uliokuwa umeongezwa ulikuwa dakika nne tu.
Hii inajenga mazingira kwamba mwamuzi alikuwa anatafuta fursa ya kuihujumu
Simba.
Baadhi ya vyombo vya habari
na washabiki walieleza pia kushangazwa na uamuzi mbaya dhidi ya Simba wakati wa
mechi kati ya Simba na Azam. Maonevu haya ya wazi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi
yameanza kuutia wasiwasi uongozi, wachezaji na washabiki wa klabu.
Kupitia taarifa hii, tunaomba
vyombo husika vimchunguze mwamuzi huyu na kuangalia uchezeshaji wake na
hatimaye achukuliwe hatua zinazostahili.
Kwa taarifa hii, tunamwomba
Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi, aangalie namna bora ya kuboresha viwango vya
waamuzi wa Tanzania kwani kwa sasa wengi wanatia aibu na ndiyo maana taifa letu
sasa limeshindwa kutoa waamuzi kwenda kwenye mashindano au mechi kubwa za
kimataifa.
Klabu ya Simba inasisitiza
kwamba haitamuonea mwamuzi ambaye ametimiza wajibu wake lakini haitasita
kumshutumu au kusema ukweli bila kupindisha pale ambapo uamuzi mbovu unaathiri
matokeo ya mechi.
KUHUSU FUJO ZILIZOTOKEA
Kwa niaba ya uongozi wa
Simba, Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, anapenda kuomba radhi kwa
TFF, Serikali, uongozi wa Uwanja wa Taifa na wadau wa soka kutokana na vitendo
vya uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali vilivyofanywa na baadhi ya washabiki
wa Simba katika pambano la jana.
Rage alisema fujo za jana
zilimshtua hata yeye kwa vile wapenzi wa Simba, kwa tabia, hawapendi vurugu na
wamekuwa na utaratibu wa kawaida wa kuwapigia makofi wachezaji hata pale timu
inapofungwa.
Kilichotokea jana, kwa mujibu
wa Rage, ni jambo la aina yake na linalotakiwa kufanyiwa tafakari jadidi
kubaini nini haswa kilikuwa chanzo na muktadha wa yaliyotokea.
Hata hivyo, amesisitiza Rage,
hakuna maelezo yoyote yanayoweza kutolewa kutetea sababu za uharibifu wa mali
na uvunjifu wa amani uliotokea na ametoa wito kwa wana Simba kujiepusha na
kufanya vitendo kama hivyo katika siku za usoni.
Uongozi wa Simba uko tayari
kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa lengo la kuhakikisha kwamba fujo
katika viwanja vya soka zinakomeshwa ili watu wazidi kwenda viwanjani badala ya
kubaki majumbani wakihofia vurugu.
TIMU
Wachezaji wa Simba wamepewa
mapumziko ya siku mbili mara baada ya mechi ya jana na wanatarajiwa kuingia
kambini Jumatatu ijayo kujiandaa na mechi ya Jumatano ijayo dhidi ya Ashanti
United itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

0 Comments