Ticker

6/recent/ticker-posts

MVELLA AJIONDOA KWENYE UCHAGUZI TFF

Na.Boniface Wambura,IMEWEKWA SEPT. 12,2013 SAA 11:35 jioni
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Eliud Mvella amejiondoa kwenye mchakato wa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Mvella amemwandikia barua Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni akielezea uamuzi wake huo pamoja na mambo mengine umetokana na kile
alichodai kuwa Kamati hiyo haikumtendea haki kwa kumwondoa.

Mbwezeleni amekiri kupokea barua hiyo, na kuongeza kuwa licha ya uamuzi huo wa Mvella aliyekuwa ameomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Saba ya mikoa ya Iringa na Mbeya, bado suala lake litasikilizwa na Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.

Kamati ya Mbwezeleni ilimuondoa Mvella katika kinyang’anyiro hicho kwa kushindwa kuheshimu Kanuni za Uwajibikaji wa Pamoja (collective responsibility) baada ya kushiriki kufanya uamuzi ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF bila ya kutaka msimamo wake wa kupinga uwekwe kwenye muhtasari na baadaye kuupinga uamuzi huo akiwa kwenye uongozi wa mkoa. 

TEMEKE, MJINI MAGHARIBI KUCHEZA NUSU FAINALI COPA
Temeke na Mjini Magharibi zinapambana kesho (Septemba 13 mwaka huu) katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zimetinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao za robo fainali ya michuano hiyo zilizochezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) asubuhi kwenye uwanja huo huo.

Wakati Temeke imetinga hatua hiyo baada ya kuilaza bao 1-0 Iringa lililofungwa dakika ya 18 na Ramadhan Mohamed, Mjini Magharibi imeing’oa Mtwara kwa ushindi wa bao 1-0.

Robo fainali nyingine zinachezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) jioni kwa Kilimanjaro kuvaana na mabingwa watetezi Morogoro huku Arusha ikioneshana kazi na Ilala.

Post a Comment

0 Comments