Mtandao rasmi wa klabu ya Azam umeandika Yeboah mwenye umbo kubwa la kimpira na urefu wa wastani anaungana na kipa kutoka Hispania, Juan Jesus Gonzalez, ambao wote wataanza kujaribiwa katika mazoezi ya Azam FC ya kujiandaa na msimu ujao yatakayoanza rasmi kesho Alhamisi saa 2.30 asubuhi.
Kipa huyo aliyekuwa akikipiga katika timu ya KSV Oostkamp ya Ubelgiji, amewahi pia kukipiga nchini Ufaransa ndani ya vikosi vya Bastia na Dijon huku akianzia soka lake kwa miamba ya Ivory Coast, Asec Mimosa’s.
Wakati akiwa Mimosas, aliwahi kuwa nahodha wa beki kisiki wa kati wa Azam FC, Pascal Wawa kabla ya beki huyo kutimkia kwa miamba ya Sudan, El Merreikh, pia amewahi kufanya kazi na kipa wa Simba, Vincent Angban, ambaye alifanikiwa kumweka benchi na kisha kutimkia Ufaransa.
Yeboah pia amewahi kuchezea kikosi cha timu ya Taifa ya Ivory Coast kilichoshiriki Kombe la Dunia Afrika Kusini mwaka 2010 na fainali za Mataifa ya Afrika 2013 nchini humo, kilichoundwa na mastaa wengine kama vile Didier Drogba, Didier Zokora, Kolo Toure, Yaya Toure, Solomon Kalou, Aruna Dindane, Emmanuel Eboue.
Akizunguma kwa ufupi na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz wakati akiwasili nchini jana na kupokelewa na Meneja wa Azam FC, Luckson Kakolaki, Yeboah alisema kuwa amekuja akiwa na fiti na kazi yake ni moja tu kuhakikisha anashinda changamoto zote na kusajiliwa na timu hiyo.
“Kwanza siku zote mimi huwa napenda sana upinzani na nimekuja hapa nikiwa kamili kukaniliana na hilo, mashabiki watafurahi wenyewe nikifanikiwa kubaki hapa,” alisema.
Baadhi ya dondoo za kiwango chake, ni uwezo wake mkubwa wa kuzuia michomo, kuusoma mchezo pamoja na mawasiliano mazuri na walinzi wake akiwa langoni, ambapo kutokana na kipaji chake cha hali ya juu aliwahi kufananishwa na gwiji wa zamani wa Ivory Coast, Alain Gouamene.
0 Comments