Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF),
limeipiga faini ya dola 5,000 Klabu ya Young African kwa kosa la
kuchelewesha
mchezo baada ya wachezaji wake kumzonga mwamuzi wakati
mchezo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho dhidi
ya GD Sagrada Esperanca uliofanyika Angola Mei 18, 2016.
Uamuzi wa mchezo huo Na. 100 ulifanywa na Kamati
ya Nidhamu ya CAF inayoundwa Mwenyekiti Raymond Hack – Raia wa Afrika
Kusini na wajumbe Mustapha Samugabo (Burundi) na Gbenga Elegbeleye
(Nigeria). Pia alikuwako Amina Kassem kutoka Sekretarieti ya CAF ambaye
ni Mtawala katika Kitengo cha Nidhamu.
Katika mkutano huo uliofanyika Cairo, Misri –
Makao Mkuu ya CAF, Julai 3, 2016, kamati ilipitia taarifa zote za mchezo
na kufikia uamuzi wa kuipiga faini Young Africans.
Taarifa za mchezo zinasema, wachezaji wa Young
Africans walionyesha utovu wa nidhamu kwa kumzonga mwamuzi na kumsukuma
mara baada ya kutoa adhabu ya penalti kwa wapinzani. Kwa tukio hilo,
mchezo huo ulisimama kwa dakika sita. Polisi waliingia uwanjani
kudhibiti hali hiyo.
Kwa kosa hilo, Wachezaji wa Young Africans
walivunja Ibara ya 82 inayozungumza utaratibu wa mawasiliano. Kwamba
chama chochote cha mpira wa miguu, klabu, ofisa au mtu yoyote wakiwamo
wachezaji, lazima waheshimu utaratibu za kuvumilia, uadiliufu na
uanamichezo.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo ya Nidhamu ya CAF, Young
Africans ilistahili kutozwa faini ya dola 10.000 za Marekani kwa makosa
ambayo si uungwana kwenye soka yaliyoonyeshwa na wachezaji wake.
Lakini kwa kuwa Young Africans haikuonyesha utovu
wa nidhamu katika mchezo mingine ya kimataifa iliyofuata dhidi ya MOB ya
Algeria na TP Mazembe ya DRC, imepunguziwa adhabu na sasa wametakiwa
kulipa dola 5,000 za Marekani kama faini. Faini hiyo haina budi kulipwa
mara moja. Na imetakiwa kuendelea kuwa na nidhamu, vinginevyo adhabu
hiyo itawarudia.
Tayari Young Africans imepewa namba za akaunti ya
CAF inakotakiwa kulipa, lakini pia imepewa fursa ya kukata rufaa kama
wataona kuna haja ya kufanya hivyo. Muda wa kukata rufaa ni siku tatu
baada ya kupewa taarifa hiyo kwa maandishi.
0 Comments