Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke siku ya jumatatu tarehe 11 mwezi huu,imetoa taarifa ya
utekelezaji wa majukumu katika katika wilaya hiyo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2016.
utekelezaji wa majukumu katika katika wilaya hiyo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Taasisi hiyo iliyopo eneo la Chang'ombe jijini Dar es salaam,Mkuu wa TAKUKURU Temeke Bi.Pilly Mwakasege amesema katika kipindi cha miezi mitatu (3)ofisi hiyo imepokea jumla ya malalamiko 52 yakiwemo ya vitendo vya rushwa na malalamiko mengineyo kutoka kwa wananchi.
![]() |
| PILLY MWAKASEGE MKUU WA TAKUKURU (M) TEMEKE AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI(HAWAPO PICHANI) |
Bi.Pilly Mwakasege amesema kati ya malalamiko 52 yaliyopokelewa na ofisi ya TAKUKURU Temeke kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2016, eneo linaloongoza kwa kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ni Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, ambapo jumla ya malalamiko 17 yalipokelewa, na kufanyiwa kazi.
"Eneo linalofuata kwa kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ni sekta binafsi (makampuni mbalimbali) ambapo ofisi imepokea malalamiko kumi (10), ikifuatiwa na Jeshi la polisi, kitengo cha usalama barabarani malalamiko nane (8 ), na idara nyingine ni Mahakama ikiwa na malalamiko (6) yaliyopokelewa na yote yanaendelea kufanyiwa uchunguzi' alisema Bi.Pilly Mwakasege.
Aidha Bi.Pilly Mwakasege ameongeza kuwa Dawati la Elimu kwa umma la TAKUKURU wilaya ya Temeke,katika kipindi hiki imetoa Elimu ya mapambano dhidi ya Rushwa kwa njia mbalimbali,ikiwemo pamoja namkutano mmoja (1) na semina kumi na moja (11) zilizoandaliwa na TAKUKURU Temeke,huku akitaja makundi yaliyopatiwa elimu hiyo ni pamoja na madereva bodaboda na bajaji,wanafunzi wa shule za Sekondari,watumishi wa idara ya Afya na wajumbe wa kamati za maendeleo ya kata pamoja na wananchi kwa ujumla.
Pia Bi.Pilly Mwakasege ameelezea mbalimbali waliyojiwekea ofisi ya TAKUKURU (M) Temeke Katika kutekeleza mapambano dhidi ya rushwa ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano ya mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
"Lengo la kwanza (1) ni kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora katika maeneo yote yanayolalamikiwa.La pili (2)ni Kuendelea kufanya uchambuzi wa mfumo katika utendaji kazi wa taasisi na idara mbalimbali za serikali ili kudhibiti mianya ya rushwa katika utoaji huduma kwa jamii na kuhakikisha maazimio yaliyowekwa baina ya TAKUKURU na idara husika yanatekelezwa kwa wakati.Lengo la Tatu (3) ni Kufanyia kazi malalamiko yote yanayohusiana na rushwa kwa wakati na weledi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria mbalimbali.Na lengo la nne (4) Ofisi ya TAKUKURU Temeke ina mkakati wa kusogeza huduma kwa mwananchi kwa kuwawekea masanduku ya maoni ili wananchi wapate fursa ya kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa kwa wakati". alisema Bi.Pilly Mwakasege
Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Temeke imepokea jumla ya Taarifa/malalamiko 52 yakiwemo ya vitendo vya rushwa na malalamiko mengineyo kutoka kwa wananchi katika kipindi cha miezi mitatu (3). Malalamiko hayo yamepokelewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi kufika ofisini, kupitia vyombo vya habari, taarifa mbalimbali za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na taarifa za kiintelijensia kupitia kwa maafisa wa TAKUKURU na watu wengine. Taarifa hizo zimefanyiwa kazi kwa kufungua majalada ya uchunguzi 24 ambayo kati ya hayo, majalada 8 yanaendelea na uchunguzi wa kina na 16 yanaendelea na uchunguzi wa awali ili kubaini makosa ya rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani pale makosa ya rushwa yatakapothibitika. Aidha taarifa 28 ambazo zilipokelewa na kuonekana kuwa zinatokana na wananchi kutoelewa utaratibu wa kiutendaji katika idara mbalimbali za serikali, wananchi walishauriwa utaratibu wa kufuata, pia TAKUKURU Temeke ilielekeza idara husika kuzitolea ufafanuzi na ufumbuzi wa malalamiko husika.
Ofisi ya TAKUKURU (M) Temeke pia ilifanya utafiti mdogo na uchambuzi wa mfumo kuhusu utendaji kazi wa askari polisi wa usalama barabarani katika maeneo ya kituo cha mabasi yaendayo Lindi na Mtwara kilichopo Mbagala Temeke. Uchambuzi huo wa mfumo ulifanyika baada ya kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa madereva wa mabasi yaendayo Lindi na Mtwara, wakiwalalamikia askari wa usalama barabarani kwa vitendo vya rushwa.
Katika uchambuzi huo wa mfumo ilimebainika kuwepo kwa mianya ya rushwa katika utendaji kazi kati ya polisi wa usalama barabarani na madereva wa mabasi. Kufuatia uchambuzi huo wa mfumo, Ofisi iliandaa kikao cha udhibiti baina ya Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani, wamiliki pamoja na madereva na kupitisha maazimio kuwa magari yote yafanyiwe ukaguzi, askari polisi wa usalama barabarani wasikae kituo kimoja kwa muda mrefu na watumishi wafanye kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni ili kuondokana na tatizo la kujihusisha na vitendo vya rushwa katika Jeshi la Polisi.
Aidha, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2016, TAKUKURU Temeke imefungua jumla ya mashauri mawili mapya mahakamani:-
i. Shauri la Jinai Na. 79/2016 - linawahusu ZAKARIA MBEDULE ambaye ni Muhasibu wa Manispaa ya Temeke, MWANAHAMIS KHALFAN ambaye alikuwa Karani wa Benki ya NMB tawi la Msasani na BERNAD MNDOLWA aliyekuwa Mkurugenzi wa IGODEN CO LTD, wameshitakiwa kwa kosa la kuiba fedha za makusanyo ya mapato ya Manispaa ya Temeke na kuyaingiza katika akaunti ya kampuni binafsi na kuisababishia Serikali hasara kiasi cha Sh.37,500,000/=, ambalo ni kosa chini ya Kifungu cha 31( Matumizi mabaya ya madaraka) cha Sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 na Kifungu cha 384 (Kushirikiana kutenda kosa), 311( Kupokea mali ya wizi), 258 na 270 (Wizi kwa Mtumishi wa umma) vya Sheria ya Kanuni za adhabu Sura Namba 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Shauri hili limefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke.
ii. Shauri la Jinai Na. 39/2016 - linamhusu BENAYA KAPINGA ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbagala Kuu Temeke, ambaye anatuhumiwa kuomba na kupokea rushwa sh. 130,000 kutoka kwa wanakikundi cha JITUME UTOBOE ili awapitishie maombi yao ya kusajili kikundi chao, kinyume na Kifungu cha 15 (Hongo na vitendo vya rushwa) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007. Shauri hili limefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke.
Aidha, hadi kufikia Mwezi Machi 2016 jumla ya mashauri 13 yanaendelea kusikilizwa mahakamani yakiwa katika hatua mbalimbali, ambapo kati ya hayo, mashauri manne (4) yanahusu idara ya Elimu, matatu( 3) uhasibu, Afya moja (1), Ardhi moja (1), Mgambo moja (1), Serikali za Mitaa moja (1), na Binafsi moja (1).
Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2016, mashauri ya Jinai matano (5) yametolewa maamuzi mahakamani, ambapo TAKUKURU Temeke imeshinda mashauri mawili(2) ambayo ni haya yafuatayo:-
i. Shauri la Jinai Na. 624/2011 lililofunguliwa tarehe 1/8/2011 katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mbele ya Mheshimiwa hakimu HAMSINI, washitakiwa walikuwa ni Bw. STANFORD ambaye ni mtumishi wa Tanesco na EMANUEL MBIFILE ambaye ni fundi mchundo TANESCO, ambao kwa pamoja walikuwa wakishtakiwa kwa kosa la Kuomba na Kupokea Rushwa chini ya Kifungu cha 15 Sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007. Shauri hili lilifikia ukomo kwa kusomwa hukumu tarehe 5/2/2016 ambapo mshtakiwa EMANUEL MBIFILE alikutwa na hatia na kupatiwa adhabu ya kifungo cha nje na mshitakiwa STANFORD aliachiwa huru.
ii. Shauri la Jinai Na. 98/2014 lililofunguliwa tarehe 19/6/2014 katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mbele ya Mheshimiwa hakimu VICKY MWAIKAMBO, mshitakiwa alikuwa ni Bw. ALLY SAID GOKO aliyekuwa mtumishi wa muda Manispaa ya Temeke upande wa Ugavi, alishitakiwa kwa kosa la kuiba vitabu vya kukusanyia mapato na kutumia vitabu hivyo kwa manufaa yake binafsi ambapo aliisababishia Serikali hasara ya Tshs. 21,214,800 ambalo ni kosa chini ya kifungu cha 258, 265 ( Wizi) na 333,335,337 (kugushi) na 284 s cha Sheria ya Kanuni za adhabu Sura Namba 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Shauri hili lilifikia ukomo kwa kusomwa hukumu tarehe 21/03/2016 ambapo mshtakiwa alikutwa na hatia na kupatiwa adhabu ya kifungo cha miaka saba (7) au faini ya shs. Milioni nne (4).
Aidha mashauri matatu (3) ambayo Watuhumuiwa waliachiwa huru ni ya haya yafuatayo:-
i. Shauri la Jinai Na. 655/2012 lililofunguliwa tarehe 29/6/2012 katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mbele ya Mheshimiwa hakimu SUZAN KIHAWA, washitakiwa walikuwa ni Bw. JUMA NASSOR ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Mzinga na Bw. SAID SHAZI ambaye alikuwa mjumbe wa Serikali za Mitaa Mzinga, ambao walishitakiwa kwa kula fedha Sh. 9,301,700/= za fidia za wananchi wa Kata ya Kibada ambao maeneo yao yalipitiwa na mradi wa umeme, ikiwa ni kosa chini ya kifungu cha 28 (ubadhirifu) na 31 (matumizi mabaya ya madaraka) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007. Shauri hili lilifikia ukomo kwa kusomwa hukumu tarehe 27/1/2016 ambapo washitakiwa wote wawili waliachiwa huru.
ii. Shauri la Jinai Na. 138/2013 lililofunguliwa tarehe 27/6/2013 katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mbele ya Mheshimiwa hakimu MWAMBAPA, mshtakiwa alikuwa LEVINA SHIRIMA ambaye ni Muhasibu Manispaa ya Temeke kwa kosa la kutopeleka benki fedha za makusanyo ya mapato aliyoyapokea ambapo aliisabishia serikali hasara ya Tshs.3,434,235/= ikiwa ni kosa chini kifungu cha 28 (1) (ubadhirifu) . Shauri hili lilifikia ukomo kwa kusomwa hukumu tarehe 27/1/2016 ambapo mshtakiwa aliachiwa huru na Takukuru Temeke imekata rufaa kufuatia hukumu iliyotolewa.
iii. Shauri la Jinai Na. 150/2013 lililofunguliwa tarehe 6/7/2013 katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mbele ya Mheshimiwa hakimu MWAMBAPA, mshtakiwa alikuwa LAURIAN J. MUNA ambaye ni Mchumi Manispaa ya Temeke kwa kosa la kuomba fedha za kuendesha Semina kwa siku tano (5) lakini semina ilifanyika siku moja hivyo kujipatia kiasi cha Tshs.1,500,00/= ikiwa ni kosa chini kifungu cha 22 (Kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri) na 28 (ubadhirifu). Shauri hili lilifikia ukomo kwa kusomwa hukumu tarehe 27/1/2016 ambapo mshtakiwa aliachiwa huru.
TAKUKURU imeendelea kutoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano ili kuondoa tatizo la kero ya rushwa nchini. Vilevile, kuwatahadharisha kwamba rushwa haitavumilika.


0 Comments