Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.March.07,2016 SAA 12:37 JIONI
Timu ya Tanzania ya mpira wa magongo (HOCKEY) chini ya umri wa miaka 21 kwa wavulana na wasichana, hii leo imekabidhiwa bendera tayari kwa safari ya kuelekea nchini Namibia, kwa ajili ya michuano ya Afrika ya vijana iliyopangwa kuanza March 18.
Michuano hiyo kwa vijana chini ya umri wa miaka 21, pia itatumika kama sehemu ya kufuzu fainali za dunia za mpira wa magongo ambazo zimepangwa kufanyika mjini Santoago nchini Chile baadae mwaka huu.
Shughuli ya kukabidhi bendera kwa timu ya taifa ya mpira wa magongo, imefanywa na Waziri wa Habari,sanaa,utamaduni na Michezo, Nape Nnauye ofisini kwake mapema hii leo.
Nape amesema wizara yake inatambua michezo yote kwa ujumla na ndio maana inaamini mchezo huo wa (Hockey) mpira wa magongo una kila nafasi ya kufanya vyema katika Nyanja ya kimataifa.
Hata hivyo Nape Nnauye ameonyesha kuwa na matumaini ya mafanikioo katika mchezo huo, kwa kujipa muda wa kuamini zao la vijana mbalo linakwenda kupambana nchini Namibia kama litaendelezwa vyema, litakua na kila sababu ya kuibeba Tanzania katika miaka ya usoni.
Katika hafla ya kukabidhi bendera kwa timu ya taifa ya Mpira wa Magongo, maafisa wa benki ya NMB nao walihudhuria kwa ajili ya kuendeleza ufadhili wa vifaa pamoja na safari kwa timu hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri wa Habari,sanaa,utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, amewataka wachezaji wanaunda timu ya vijana ya mpira wa magongo kutambua umuhimu wa wajibu wao katika michuano ya vijana ya Afrika, hivyo wanapaswa kwenda kupambana watakapokua nchini Namibia.
Naye mwenyekiti wa chama cha mpira wa magongo nchini Tanzania Abraham Sykes ametoa shukrani zake kwa makocha wa mchezo huo, Waziri wa Habari,sanaa,utamaduni na Michezo kwa kukabidhi bendera, pamoja na kampuni ya NMB kwa kufanikisha safari ya timu ya taifa.
Sykes pia ametoa wosia kwa wachezaji wanaopunda timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 21 ambao wataondoka nchini March 13 kuwa na nidhamu wakati wote wa michuano ya Afrika ili kufanikisha azma ya kupambana vilivyo na ikiwezekana kurejea nchini wakiwa mbingwa.
Kwa upande wa ofisa mkuu wa fedha wa benki ya NMB, Waziri Barnabas, amesema wao kama kampuni wanathamini sana michezo, na ndio maana wameamua kusaidi kwa upande wa vifaa pamoja na usafiri wa kwenda na kurudi kwa timu ya taifa ya vijana ya mpira wa magongo.
Barnabas pia ametoa wito kwa wachezaji, kwa kuwataka kuwa na ari ya kushindana wakati wote, huku wakitambua watanzania wana kiu ya kuona mafanikio yanapatikana katika michezo bila kujali aina ya mchezo.
Wakati huo huo kocha mkuu wa timu ya mpira wa magongo Varentina Quaranta, amesema pamoja na kikosi chake kusheheni wachezaji wengi wenye umri mdogo, bado anaamini watakwenda kushindana kutokana na maandalizi waliyoyafanya huku akiwataka watanzania kuiamini na kuombea timu hiyo ya vijana chini ya umri wa miaka 21.
Nao wachezaji wamesisitiza kuwa katika ari ya kwenda nchini Namibia kupambana kwa nguvu zao zote na wanaamini kama mambo yatakwenda vyema, basi wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

0 Comments