Ticker

6/recent/ticker-posts

HII NDIO SABABU YA KUSITISHA MKATABA WA KOCHA WA YANGA BRANDTS

  Mhariri:Herman Kihwili.IMEWEKWA DESEMBA 23.2013 SAA 07:40 MCHANA
Uongozi wa klabu ya Young Africans SC umempatia taarifa (Notice) ya siku ya thelathini (30) kocha mkuu mholanzi Ernie
Brandts juu ya kusitisha mkataba wake kuanzia jana Disemba 22 mwaka huu.
Akizungumza na waandihi wa habari mapema leo hii Mwenyekiti - Kamati ya Mashindano Abdallah Bin Kleb, amesema uamuzi huo umefuatia muenendo wa matokeo mabaya katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza la Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC mwishoni mwa wiki.
"Hatua ya Young Africans SC kusitisha huduma na Brandts isichukuliwe kama chuki bali ni moja ya sehemu ya kuhakikisha tunaboresha benchi la ufundi ili tuweze kupata matokeo mazuri katika Mashindano yanayotukabili"alisema Abdallah Bin Kleb.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Abdallah Bin Kleb (katikati) akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani) makao makuu ya klabu ya Yanga, kushoto ni Musa Katabaro na kulia Afisa Habari Baraka Kiziuguto
Aidha Abdallah Bin Kleb ameongeza kuwa,ukiangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga SC na wapinzani wao Simba, na soka walilolocheza kwenye mchezo wa mwishoni mwa wiki ni dhahiri mwalimu amefikia mwisho kimbinu na hana njia mbadala.
"Young Africans SC imekua ikicheza chini ya kiwango katika michezo ya Ligi Kuu hali iliyopelekea kupata ushindi kwa tabu na wakati mwingine timu kupoteza pointi."
"Kufuatia kupewa taarifa ya siku 30, Brandts ataamua mwenyewe kama ataendelea kusimamia mazoezi ya timu au kuondoka moja kwa moja kabla ya muda huo ukiwa haujakamilika."
 Bin Kleb amesema kama Brandts ataondoka mapema timu itaendelea na mazoezi kama kawaida kila siku asubuhi katika uwanja wa bora kijitonyama ili kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa chini ya kocha msaidizi Fred Felix “Minziro”.
"Ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano ya kimataifa uongozi unakamilisha maandalizi ya safari ya kambi nje ya nchi na taratibu zote zitakapokamilika tutawajulisha."alifafanua Bin Kleb
Hata hivyo uongozi wa Yanga upo katika mchakato wa kumapata mrithi wa Brandts ambaye ataungana na timu kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili na Mashindano ya klabu Bingwa Afrika.
Pia Abdallah Bin Kleb ametumia nafasi hii kuwaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa Yanga wasivunjike moyo kufuatia matokeo ya bonanza la Nani Mtani Jembe lililofanyika mwishoni mwa wiki,na amesema uongozi unajipanga kuhakikisha timu hiyo inaimarika kwenye benchi la ufundi na kurudisha furaha katika mzunguko wa pili wa VPL.

Post a Comment

0 Comments