IMEWEKWA SEPT 10,2013 SAA 2:10 USIKU
Mwanamume mmoja raia wa Afrika Kusini aliyekuwa
anakabiliwa na tishio la kufukuzwa kutoka New Zealand kwa kuwa mnene
kupita kiasi,ameongezwa muda wa miezi 23 kuendelea kuishi nchini humo.
Hata hivyo,Albert Buitenhuis hatapokea huduma ya bima ya afya ya serikali.
Albert ambaye ni mpishi wa hoteli,
ana uzani wa kilo 130 na alikata rufaa miezi miwili iliyopita baada ya
ombi lake la kutaka apewe viza mpya ya kumwezesha kufanya kazi nchi humo
kukataliwa kwa misingi kuwa afya yake sio nzuri.
Amepunguza kilo 30 tangu kuhamia mjini Christchurch miaka sita iliyopita.
Naibu waziri wa uhamiaji Nikki Kaye alisema kuwa
sababu kuu ya ombi la Bwana Buitenhuis kukataliwa ni ugonjwa alionao
kwenye magoti yake.
Hata hivyo, aliwapa muda zaidi Bwana Buitenhuis
na mkewe Marthie, wa kuweza kuishi nchini humo baada ya kusema kuwa
itambidi agharamie matibabu yake mwenyewe.
Aidha Bwana Buitenhuis, aliyeandika kuhusu
masaibu yake kwenye blogu, alisema kuwa hatua ya serikali imeleta hisia
mchanganyiko kwake.
Buitenhuis, ameahidi kupunguza kilo nyingine 25
ingawa kwa sasa anasema kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi kwani
hawana pa kuishi.
New Zealand ni moja ya nchi yenye idadi kubwa ya watu walio wanene kupita kiasi.
Idara ya uhamiaji imesema kuwa ni muhimu kuwa
wahamiaji wote wawe na hali ya kiafya inayokubalika ili kuipunguzia
serikali gharama ya kutibu wagonjwa.
Chanzo:BBC SWAHILI

0 Comments