Na.Boniface Wambura,IMEWEKWA SEPT. 13,2013 SAA 11:45 jioni
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu ilipokabidhi Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) katika
mzunguko wa pili msimu uliopita.
Amesema
TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi kwa lengo la kutaka klabu
zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo limeleta
mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa marefa na
makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
“Fedha
za udhamini sasa zinakwenda moja kwa moja kwenye Kamati ya Ligi. Ni
matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani tumeanzisha jambo hili
kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema Rais Tenga
wakati akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali vya
habari.
Rais
Tenga amesema mahali penye utulivu na utawala bora watu wanakuwa na
imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni lazima kwa kampuni kuwekeza
kwa vile kunakuwa hakuna vurugu.
Amesema
ukiondoa Afrika Kusini na Angola katika ukanda huu wa Afrika Mashariki,
Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo yenye udhamini mkubwa
kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo ya televisheni.
Pia
amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za Ligi Kuu hazitaruhusiwa
kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti zao za mapato na
matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika zijiandae
kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.
Kuhusu
tiketi za elektroniki, Rais Tenga amesema bado linafanyiwa kazi na CRDB
ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na liko katika hatua nzuri, kwani
nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza haraka iwezekanavyo.
“Tiketi
za elektroniki zimechelewa kuanza kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika,
lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu katika karibu viwanja vyote.
Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer (mashine za kuchapia),
zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa Taifa, system
(mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa tunaangalia
uwezekano wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa Taifa
una system yake tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala
lisitucheleweshe,” amesema.
WACHEZAJI 620 WATHIBITISHIWA USAJILI FDL
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imethibitisha usajili wa wachezaji 620 kati ya 624 wa
timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza kutimua vumbi kesho
(Septemba 14 mwaka huu).
Wachezaji
wanne ambao usajili wao umezuiwa mpaka watakapokamilisha taratibu ni
Emmanuel Simwanza Namwando wa African Lyon, Godfrey Bonny Namumana
(Lipuli FC), na Enyinna Darlington na Chika Keneth Chukwu wote wa Mwadui
FC ya Shinyanga.
Darlington
na Chukwu ambao wote ni Wanigeria wamezuiwa mpaka watakapowasilisha
vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji wakati Namumana
aliyekuwa akicheza nchini Nepal bado hajapata Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC).
Nayo
African Lyon imetakiwa kufikia muafaka na AYOSA Academy ambayo Namwando
anatoka juu ya usajili kabla ya kuanza kumtumia mchezaji huyo.
Klabu
ambazo zimemaliza nafasi zote 30 usajili katika FDL ni Friends Rangers
FC ya Dar es Salaam, na Stand United FC ya Shinyanga wakati iliyosajili
wachezaji wachache zaidi ni Burkina Faso FC. Klabu hiyo ya Morogoro
imesajili wachezaji 19 tu.
Vilevile
Kamati hiyo vilevile imethibitisha usajili wa wachezaji wanane wa klabu
za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) waliosajiliwa katika hatua ya pili ya
usajili iliyoanza Agosti 14 hadi 30 mwaka huu.
Wachezaji
hao ni Samir Ruhava na Amani Simba (Ashanti United), Robert Machucha na
Said Ndutu (Yanga U20), Ayoub Masoud na Abdallah Selemani (Coastal
Union U20), Ramadhan Kipalamoto (Simba U20) na Henry Joseph (Simba)
ambaye tayari Hati yake Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imeshawasili.

0 Comments