Mhariri:Herman Kihwili. IMEWEKWA.JAN 13.2016 SAA 12:56 JIONI
Michuano ya kuwania Kombe la Shirikisho ya Azam (Azam Sports
Federation Cup 2016/2017), inatarajiwa kuendelea kesho kwa
kukutanisha
timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya hatua ya kushirikisha timu
za daraja la pili na timu za ligi ya mikoa (RCL) kukamilika.
Kesho Jumamosi Januari 14, mwaka huu, KMC ya Kinondoni itacheza na
Kiluvya United ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kabla ya
keshokutwa Jumapili Januari 15, mwaka huu kwenye viwanja tofauti.
Mechi nyingine za Jumapili ni kati ya Ashanti United na Friends
Rangers – zote za Dar es Salaam mchezo utakaofanyika Uwanja wa Karume
ulioko Ilala jijini wakati Coastal Union itacheza na Mgambo JKT kwenye
Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Panoni ya Kilimanjaro itaikaribisha African Sports ya Tanga kwenye
Uwanja wa Ushirika Moshi wakati Alliance itacheza na Pamba kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba jijini Mwanza huku Mbeya Warriors ikiikaribisha Kimondo
kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Kurugenzi itacheza na Kiluvya kwenye Uwanja wa Mafinga wakati kwenye
Uwanja wa Karume Musoma, Rhino ya Tabora itakuwa mgani wa Polisi Mara
ilhali Singida United itakuwa mwenyeji wa Mvuvumwa ya Kigoma kwenye
Uwanja wa Namfuta.
Polisi ya Morogoro itacheza na timu nyingine ya Polisi kutoka Dodoma
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati kwenye Uwanja wa Njombe,
Njombe Mji itacheza na JKT Mlale kutoka Songea wakati Polisi Dar
itacheza na Mshikamano Jumatatu ya Januari 16, mwaka huu.
Kwa mechi zilizocheza jana Januari 12, 2017 Madini ya Arusha ambayo
iliilaza Mirambo ya Tabora mabao 4-0 sasa itaivaa Oljoro iliyoshinda kwa
penalti 4-3 dhidi ya Mawenzi baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya
bila kufungana. Mechi hiyo itafanyika kesho kwenye Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid mjini Arusha.
Timu zilizotangulia na kusubiri washindi wa michezo ya leo ni Kabela
City ya Shinyanga ambayo iliifunga Murusagamba ya Kagera mabao 4-0
katika mchezo uliofanyika Kahama huko mkoani Shinyanga.
Kwa hiyo, Kabela City sasa inasubiri mshindi kati ya Jangwani ya
Rukwa na Stand Bagamoyo ya Pwani ambazo zinacheza leo Januari 13, mwaka
huu katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mandela ulioko Msata mkoani
Pwani.
Timu nyingine iliyotangulia ni Changanyikeni ya Dar es Salaam
iliyoifunga Burkina Faso ya Morogoro bao 1-0 katika mchezo uliofanyika
Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Changanyikeni sasa inasubiri
mshindi kati ya Green Warriors ya Pwani na Cosmopolitan ya Dar es Salaam
ambazo leo zinacheza Uwanja wa Karume.
Baada ya Namungo FC ya Lindi kutojitokeza Uwanja wa Majimaji,
timu ya The Mighty Elephant ya Songea ilipewa ushindi na kwa sasa
inasubiri mshindi kati ya Mashujaa ya Kigoma ambayo leo inacheza na
Kitayosa ya Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.
0 Comments