Na.Boniface Wambura,.IMEWEKWA OCT. 22,2013 SAA 1:35 USIKU
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi
tatu; ambapo Yanga itaikaribisha
Rhino Rangers katika mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Coastal
Union inaikaribisha Simba katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Tanzania
Prisons ambayo imepoteza mechi mbili zilizopita ugenini dhidi ya
Ashanti United na Simba inarejea uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine
kwa kuikaribisha Kagera Sugar.
Nayo
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa
mechi moja ya kundi A itakayozikutanisha Tessema na Villa Squad kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
SERENGETI BOYS YAALIKWA MICHUANO YA ANOCA
Timu
ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Serengeti
Boys) imealikwa kushiriki Olimpiki ya Afrika itakayofanyika Mei
mwakani.
Mpira
wa miguu ni kati ya michezo 22 itakayoshindaniwa katika mashindano
yatakayofanyika Gaborone, Botswana chini ya Kamati za Olimpiki za Afrika
(ANOCA).
Kwa
mujibu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Tanzania imepewa nafasi
ya kushiriki katika michezo hiyo ya Olimpiki kwa Afrika kutokana na
kuwa na programu nzuri za vijana hasa chini ya umri wa miaka 17.
Hiyo itakuwa ni michezo ya Pili ya Afrika kwa Olimpiki ambapo ya Kwanza ilifanyika mwaka 2010 jijini Rabat, Morocco.

0 Comments